***************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MAKATIBU wakuu wa Wizara nane wametembelea Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ikiwemo mgodi wa Calfornia Camp, EPZA Mirerani City na Tanzanite Forever Lapidary.
Katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema makatibu wakuu hao wamefika Mirerani ili kushuhudia utendaji kazi unavyoendelea.
Profesa Msanjila ametaja baadhi ya makatibu wakuu hao ni Wizara za Tamisemi, Madini, Maji, Ardhi, Nishati, Biashara, Sheria na Katiba.
“Lengo la msafara huu ni kutembelea, kukagua na kuona namna shughuli za utekelezaji wa maagizo ya serikali unavyotekeleza kwa kila upande wa Wizara mbalimbali,” amesema.
Mkurugenzi wa Tanzanite Lapidary Forever, Arafat Juma amesema wanaishukuru Serikali kwa namna wanavyoendesha shughuli ya kusimamia biashara ya madini hayo.
“Tunashukuru Serikali kwa namna inavyotupa ushirikiano wanunuzi wa madini ya Tanzanite nasi tunaahidi kuendeleza ushirikiano huo,” amesema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mary Gasper Makondo, amewapongeza wasichana wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary, wanaokata na kuongeza thamani madini ya Tanzanite.
“Tumewaona wasichana wengi wanaokata madini wakiwa na ari na wenye kujiamini kwenye sekta hii ya madini ya Tanzanite, tunawapongeza sana,” amesema.
Dkt Cutis Msosa meneja wa mgodi wa California Camp unaomilikiwa na Deo Monja ambao umetembelewa na makatibu hao amesema uchimbaji wa Tanzanite unafanyika kwa mshazari na siyo wima kama dhahabu.
Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara Mirerani Agosti 7 mwaka huu na kusisitiza biashara ya Tanzanite ifanyike Mirerani.
Rais Samia aliahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya soko kwa ajili ya biashara hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea Mirerani Julai 7 mwaka huu nakuagiza biashara ya Tanzanite ifanyike Mirerani pekee.