Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 10,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
Baadgi ya watendaji wa Wizara ya maji pamoja na waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati akizungumzia mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika eo November 10,2021 jijini Dodoma
Mwandishi kutoka Uhuru FM Sakina Abdulmasoud akiuliza swali kwa Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (hayupo pichani) leo November 10,2021 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
Mwandishi kutoka EATV Oliva Nyeriga akiuliza swali kwa Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (hayupo pichani) leo November 10,2021 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari leo November 10,2021 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI ya Maji,Jumaa Aweso amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara,wastani wa wakazi wa mijini wanaopata huduma ya majisafi na salama imeongezeka kutoka asilimia 25 ya wakazi wote wanaoishi mijini mwaka 1961 hadi kufikia wastani wa asilimia 86 mwaka 2021.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Novemba 10,2021,Jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya maji katika miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
,Waziri Aweso amesema Wizara yake imendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini na vijijini.
Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara,wastani wa wakazi wa mijini wanaopata huduma ya majisafi na salama imeongezeka kutoka asilimia 25 ya wakazi wote wanaoishi mijini mwaka 1961 hadi kufikia wastani wa asilimia 86 mwaka 2021.
“Upatikanji wa maji vijijini ni asilimia 72.3 na hali ya upatikanaji wa maji na mijini ni asilimia 86,Sisi kama Wizara tumejipanga kwa maelekezo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa maana itakapofika 2025 hali ya upatikanaji wa maji vijijini iwe 85 na mijini 95,”amesema.
Waziri Aweso amesema Miradi ya kimkakati inaendelea kutekelezwa lengo likiwa ni watanzania waweze kupata maji.
UPOTEVU WA MAJI
Kuhusu upotevu wa maji,Waziri huyo amesema wamewasainisha mikataba Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji lengo likiwa ni kuzuia upotevu wa maji.
“Katika eneo la upotevu wa maji,Wizara imefanya mageuzi ambapo Wakurugenzi wetu tumewasainisha mkataba sio bla bla kwa mfano hili suala la upotevu wa maji unaweza ukapita kwenye Mamlaka za Maji anakwambia hapa tunapoteza maji kwa ni asilimia 48,kuna wiza wa maji baadhi ya hoteli hazilipi,
Tunaendelea kuwashguhulikia niombe sana si busara kuona maji yanamwagika halafu mwanananchi hana maji,”amesema.
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuimarisha maabara za maji ili ziendelee kutoa huduma kama inavyokusudiwa.
UBAMBIKIZWAJI WA BILI ZA MAJI
Aidha,Waziri huyo amepiga marufuku ubabikizwaji wa bili za maji kwa wateja ambapo amedai ndio maana walianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)lengo likiwa ni kuondoa tatizo hilo.
“Ubambikizi wa bili za maji ndio maana wameanzisha Ewura jukumu lake ni kudhibiti bili za maji tunawataka waendelee kufuatilia.Ikitokea wakajulikana tutashughulika nao,”amesema.
USIMAMIZI WA UBORA WA MAJI
Amesema mafanikio katika eneo la usimamizi wa ubora wa maji ni pamoja na Maabara ya Maji ya Mwanza iliteuliwa mwaka 2006 na Jumuiya ya Ulaya (EU) kupima ubora wa maji yanayotumika katika usindikaji wa minofu ya samaki kabla ya kusafirishwa kwenda katika soko la Ulaya na inaendelea na kazi hiyo.
“Teknolojia ya kutumia mifupa ya ng’ombe yenye uwezo mkubwa wa kupunguza madini ya fluoride kufikia viwango ambavyo havina madhara kiafya imefanyiwa utafiti katika Maabara ya Ngurdoto Mkoani Arusha kwa muda mrefu na sasa inatumika kuwapatia Wananchi maji yenye kiwango cha fluoride kinachokubalika kitaifa,”amesema
Amesema Maabara za maji zimeendelea kutambulika kimataifa kwa kupatiwa ithibati kutokana na maboresho yaliyofanyika ambapo mpaka sasa maabara za Mwanza, Dar es salaam, Bukoba, Musoma, Kigoma, Singida na Shinyanga zimepatiwa ithibati.
MIRADI 566 KATI YA 632 YATEKELEZWA
Amesema hadi kufikia Juni 2021, jumla ya miradi 566 kati ya miradi 632, sawa na asilimia 89.6 imekamilika ambapo miradi 115 kati ya miradi 177, sawa na asilimia 65 ya miradi imeanza kutoa huduma kwa Wananchi.
“Miradi yote iliyosalia itakamilishwa ifikapo mwezi Juni 2022 ambapo katika kipindi hicho, miradi mipya 912 ya maji vijijini ambapo kati ya miradi hiyo, miradi 458 imekamilika na kuanza kutoa huduma.
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo na kuanza kutoa huduma kumeongeza wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 72.3 kufikia mwezi Juni 2021.
Amesema Hadi sasa, jumla ya vijiji 8,708 kati ya 12,327 vinapata huduma ya maji.
“kwa kipindi kirefu miradi ya maji imekuwa ikitekelezwa na kukamilika lakini haiwi endelevu katika utoaji wa huduma iliyokusudiwa hususan katika maeneo ya vijijini. Katika kukabiliana na hali hiyo, Wizara imefanya mageuzi makubwa ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji inakuwa endelevu. Mageuzi yaliyofanywa ni ya kitaasisi, kifedha na kiufundi,”amesema.
Amesema hadi kufikia Oktoba 2021, jumla ya Mamlaka 96 za Miji Mikuu ya Mikoa, Miji midogo na Miradi ya Kitaifa zimeanzishwa na zinatoa huduma ya maji hapa nchini.
MIRADI MIKUBWA
Aidha,Waziri Aweso ameitaja miradi mikubwa ambayo Wizara ya Maji inaitekeleza kuwa ni Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka miji ya Kahama na Shinyanga,
Uboreshaji wa huduma ya majisafi katika Jiji la Dar es Salaam kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini na ulazaji wa bomba kuu.
Miradi mingine ni wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka miji ya Isaka na Kagongwa,Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka miji ya Tabora – Igunga – Nzega,Mradi wa maji kwa mji wa Lindi, Miradi ya maji na usafi wa mazingira katika miji ya Mwanza, Mbeya na Iringa.
“Mradi wa maji na usafi wa mazingira mjini Kigoma,Mradi wa kusambaza maji katika maeneo ya Kibamba na Kisarawe,Mradi wa Maji wa Misungwi,Mradi wa Maji Nansio Ukerewe,Mradi wa Maji wa Longido,Mradi wa Maji wa Lamadi, Mradi wa Maji wa Bokwa na Mradi wa Maji wa Sengerema,”amesema.
Amesema miradi 26 ya maji mijini imekamilika na inatarajiwa kuzinduliwa na Viongozi wa Kitaifa.
CHANGAMOTO
Waziri Aweso amesema changamoto kubwa katika Wizara hiyo ni pamoja na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kulinda na kutunza miundombinu ili iendelee kutoa huduma endelevu kwa Wananchi mijini na vijijini.
Aidha, athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ambazo husababisha ukame, mafuriko na kupungua kwa upatikanaji wa rasilimali za maji sehemu mbalimbali nchini.
“Kwa mfano wakati tunapata uhuru idadi ya watu nchini ilikuwa milioni 10 na kila mtu aliweza kupata mita za ujazo 12,600 kwa mwaka, kiwango hiki kimepungua hadi kufikia mita za ujazo 2,250 kwa mtu kwa mwaka 2019,”amesema
MWELEKEO WA SEKTA YA MAJI
Amesema mwelekeo wa Wizara hiyo ni Kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wananchi waishio mijini inafikia zaidi asilimia 95 mwaka 2025,Kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wananchi waishio vijijini inafikia asilimia 85 mwaka 2025, na
Kuwa na Rasilimali za maji endelevu kwa kulinda, kutunza, kuendeleza na kutafuta vyanzo vipya vya maji.
“Serikali imepanga kutekeleza miradi itakayotumia vyanzo vya maji vya uhakika vikiwemo maziwa makuu ya Tanganyika, Nyasa na Victoria na mito mikubwa kama mto Ruvuma, Rufiji, Kiwira, Songwe na Kagera,”amesema.
Amesema Wizara itaendelea kuelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kuweka mkazo katika usimamizi wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Na. 11 ya mwaka 2009 na Kanuni zake ikiwemo kuwatoza faini wanaoharibu au kuchafua vyanzo vya maji.