**************************
MAKETE
Timu ya askari polisi kwa kushirikiana na vikosi vya jeshi la uhamiaji mkoa wa Njombe zimefanya msako katika kitongoji cha Isaganilo kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 18 na mtanzania mmoja aliyekuwa akijaribu kuwavusha ili kuingia nchini Malawi.
Akitoa onyo kwa wahusika wa biashara hiyo ya giza kamishina msaidizi mwandamizi wa uhamiaji mkoa wa Njombe John Yindi amesema kumekuwa na mikasa mingi ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu wakitoka nchi jirani lakini hadi sasa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuutia nguvuni mtandao wa biashara hiyo inayopingwa vikali ulimwenguni .
Kamanda Yindi amesema mafanikio makubwa waliyoyapata hivi karibuni yametokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe ambao wamekuwa wakivujisha taarifa na kwamba tabia ya kuwafichua wahusika inapaswa kuendelea kwa usalama wa wananchi na taifa kwa ujumla
“Tumefanikiwa kuwakama wahamiaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe hatua ambayo ni matokeo ya wananchi wazalendo ambao wamekuwa wakitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya uwepo wa watu wasiowatambua katika makazi yao,Amesema kamanda uhamiaji mkoa John Yindi”
Katika Operesheni hiyo Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issah amesema mamia ya wahamiaji haramu wanaokamatwa mkoani hapa wanashirikiana na watazania hivyo jeshi halita muacha salama atakaebainika kutumia chombo chake kuwavusha watu hao.
“Tumewakamata wahamiaji 18 akiwemo mtanzania mmoja ambaye alikuwa akisafirisha watu hao jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na kwamba jeshi limejidhatiti kudhibiti watu hao hadi watakapo koma,Amesema kamanda Issah
Wiki Tatu zilizopita jeshi la uhamiaji liliwakamata wahamiaji haramu 52 wilayani Wanging’ombe wakitokea nchi za ethiopia na malawi.