*****************************
10,Nov
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WAWEKEZAJI na jamii wameaswa kuchukua hatua madhubuti katika uwekezaji na matumizi ya plastic yanayosababisha uchafuzi wa Mazingira, pamoja na kudhibiti shughuli zinazosababisha mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea joto kali na kusababisha Kansa ama athari ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Aidha jamii imetakiwa kujenga Tabia ya kupanda miti ,kulinda misitu kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
Rai hiyo imetolewa na muasisi na mkurugenzi wa Partnership for Green Future (PGF) inayojihusisha kutetea changamoto zinazosababisha mabadiliko ya tabia nchi hususan uwekezaji katika gesi ya ukaa na mambo ya uchimbaji wa makaa ,Rehema Peter katika maandamano na mkutano wa kuunga mkono waliopo Scotland kwenye mkutano mkubwa wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi na kuunga mkono hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika mkutano huo mkubwa.
Alisema mkutano wao umefadhiliwa na WWF na kuratibiwa na PGF Lengo ni kupinga shughuli zinazosababisha mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha madhara.
Rehema alieleza ,wanategemea wasimamizi na watunga Sheria na sera kuunda Sheria zitakazowabana wale wote wanaosababisha madhara ya uchafuzi wa hali ya hewa na Mazingira.
“Tunapinga vikali uwekezaji na matumizi ya plastic,tunahitaji plastic iondoke, hivyo ni wakati wa kuweka nguvu kubwa kupunguza shughuli za kimaendeleo ambazo zinazozalisha cabon inayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.”alisisitiza Rehema.
Nae mratibu wa Extinction Rebellion Tanzania,Shamim Wasii Nyanda alisema nchi inahitaji uchumi ukue na kuwepo kwa maendeleo lakini inabidi viwanda viweke Mazingira ambayo yatadhibiti uchafuzi wa hali ya hewa ili kuepukana na madhara ndani ya jamii.
Aidha alikemea , utupaji wa taka ngumu, plastic ovyo ili kuweka miji safi na kulinda uchafuzi wa Mazingira.
Shamim alisema wametoa elimu ya Mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo kwa wanafunzi wakiwemo Tumbi Sekondari, Shule ya wavulana Kibaha na wadau mbalimbali.
“Mazingira yahifadhiwe na vyanzo vya maji pamoja na misitu vilindwe “”::ni wakati wa kwenda na Tanzania ya kijani kibichi ,jamii ilime na kulinda Mazingira”alisisitiza Shamim.
Ofisa elimu Sayansikimu ,Laurencia Massawe aliwataka wanafunzi kuacha kutupa makaratasi ovyo ,kuwa mabalozi kwenye jamii kuhimiza kupanda miti .
Mkazi wa Visiga ambae ni mlemavu wa ngozi Salma Ramadhani ,alisema , mabadiliko ya tabia nchi yanasababisha joto kali na kuleta athari kwenye ngozi zao na Kansa ya ngozi.
Salma aliomba pia msaada upelekwe kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum hasa wenye ulemavu wa ngozi ikiwemo kofia,mafuta maalum ya ngozi zao .