*****************************
Adeladius Makwega
Mbagala.
Siku hiyo tulijulishwa kuwa Ipogoro Iringa kunamafuriko basi wanahabari wasiku hiyo tulipanda daladala zinazoenda Caglielo na tulishuka na kilima cha Ipogoro na kufika hadi stendi ya mabasi ya Ipogoro.
Tuliofika hapo nakumbuka walikuwepo waandishi wengi. Ninawaokumbuka kwa majina ni Francis Gondwin huyu alikuwa ripota wa Redio Country FM-Iringa, nilikuwepo mimi wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa mwaka 3 wa Shahada ya Sanaa ya Habari ya Chuo cha Tumaini Iringa na nilikuwa natuma stori kwa Kampuni ya Media Solution LTD wachapaji wa THISDAY na KUlLIKONI. Alikuwepo dada mmoja anaitwa Blandina Semaganga alikuwa akitazangaza Redio Country FM na pia alikuwepo marehemu Daudi Mwangosi akiwakilisha Channel 10.
Daudi mwangosi alikuwa na ofisi yake kwenye Ghorofa la Pride ambalo wakati huo Redio Country FM ndiyo waliporushia matangazo.
Wakati huo waandishi tunapotaka kwenda kuchukua habari mwahabari wa TV anakuwa msaada mkubwa kwa mambo kadhaa kwanza anafahamika kwa kuwa Runinga inamuonesha kila siku, Pili tukiwa naye tunapata urahisi wa kupata watu tunawahoji kwani watu wanapenda kuonekana kwenye TV.
Tatu hata kupata majibu ya serikali ilikuwa nyepesi sana kuliko ukienda wewe mwenyewe mwandishi wa magazeti na redio. Nne kwa wale wanaotoa posho mkiwa na Daudi Mwangosi mnaweza kupata posho kwa wepesi sana kwa kuwa viongozi wengi wanapenda kuonekana kwenye TV.
Mkipata posho angalau inakusaidi kwa ajili ya nauli, chakula cha mchana na mambo mengine ya binafsi nyumbani kwako. Kwa kuwa hadi kulipwa posho yangu na kampuni hadi stori ziwe nyingi.
Kwa hiyo mwandishi mwenye kamera ya TV yeye ni sawa na mtu mwenye bunduki kwa wale wanaokwenda kuwinda. Japokuwa wengine mnakuwa na mishale mikuki marungu zote ni silaha lakini bunduki ndiyo kila kitu.
Tulipofika Ipogoro kila mwanahabari alitimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuwahoji waathirika wa mafuriko na viongozi wa eneo hilo. Mvua hii ilikuwa na athari kubwa hadi maji yalikaribia katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ipogoro cha wakati huo.
Tulipomaliza tukaulizana jamani tunarudi vipi mjini, mimi nikawambia mie sina nauli. Daudi Mwangosi akasema Makwega usiwe na shaka tutafika mjini lakini lazima tukaibalansi stori kwa Mkurugeniz wa Halmshauri ya Mji wa iringa wakati huo alikuwa ni Bi Theresia Mmbando.
Bi Theresia Mmbando wakati huo alikuwa ni dada mmoja mrefu, ana mwili uliojengeka, mrembo, mweupe, anajipenda sana, huku akijiamini sana na pia akiwa mkarimu kwa wageni. Kwa wale ambao wamemsahau ndiyo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye Mkoa wa Pwani alipostaafu.
Iringa vijijini walikuwa Halmashauri ya Wilaya na Mkurugenzi wake alikuwa ni Bi Tina Sekambo alikuwa mama mmoja mrefu, mweupe, anapenda sana kukata nywele, yeye alikuwa hasuki wala kuweka dawana huku akiwa mkali na ilikuwa tabu kumuona ofisini kwake.
Bi Tina Sekambo alikuwa kidogo mzito lakini Bi Theresia Mmbando alikuwa anaelewana sana na Daudi Mwangosi. Mimi niliwahi kumtani Daud Mwangosi kaka vipi mbona unapendwa sana na Mama Mkurugenzi Theresia Mmbando?Maana alikuwa akitaniwa kama mzee wa majimbo. Huku Mwangosi akisema kuwa kaka yale maji marefu siyawezi. Kwa hiyo Mwangosi alisema jambo ambalo kila mmoja(miongoni mwetu) alikuwa na uhakika nalo.
“Tufanya tufanyacho kumuwahi Bi Theresia Mmbando na yeye atatupatia chochote.”
Blandina Semaganga ambaye alikuwa amehitimu chuo cha Tumaini Iringa alikuwa kama anajitolea kupata uzoefu Redio Country FM akasema Makwega usiwe na shaka nitakupatia nauli ya kurudi hadi kwako Mwang’ng’o mbele ya Kihesa, nilimshukuru huyu dada yangu Blandina kwa kunihakikishia kunipatia nauli hiyo.
Gafla tulivyotoka tu barabarani kwa mbali ilionekana gari ya polisi Defenda inakuja basi Mwangosi akaipiga mkono na kweli polisi walikuwa wakimfahamu sana na hawakuwa na uadui wowote nayeye gari iliposimama akamwambia afande dereva tunaenda mjini tunaomba msaada. Polisi akasema twendeni nyinyi mapaparazi.
Tukaingia ndani huku akimwambia siye tunashukla Halmshauri ya Mji Iringa. Kweli vijana wa polisi walitufikisha hapo tukaenda kwa Mkurugenzi Theresia Mmbando na akatupatia kila mwandishi 15,000/. Kumbuka dada Blandina Semaganga alinipa ahadi ya kunipa pesa kwa hiyo hapo hakunipa tena. Bi Theresia Mmbando aliokoa jahazi la ndugu Makwega lililokuwa likizama.
Daudi Mwangosi akarudi katika ofisi yake Pride na mie na Dada yangu Blandina Semaganga tutaenda Country Fm kupeleka stori nakumbuka wakati huo Mhariri Mkuu na Meneja wa hii Redio alikuwa ni Mahija Zayumba sasa yupo Clouds.
Daudi Mwangosi, Mahija Zayumba na wengineo kwa elimu zao za habari kwa hakika na kwa ukweli wa Mungu walikuwa elimu za kawaida lakini walitusaidia na kutuvumilia mno mimi na Blandina Semaganga ambao tulikuwa tunakaribia kuwa na Shahada au tumehitimu.
Hata tulipokuwa tukienda ofisini za serikali namna ya kuongea na viongozi wa serikali kwa mfano mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Iringa wakati huo alikuwa mtoto Mwamwindi.
“Makwega hawa ni Halmshauri na Mkoa wanatupatia matangazo kwa hiyo namna ya kuziweka habari zao fanya hivi na fanya vile ili waendelee kutoa matangazo.” Alinifundisha Bi Mahija Zayumba.
Hata walipokuwa wakija kuchukua ripoti za Chuo cha Tumaini Iringa walikuwa wakitushirikisha namna ya kurekodi sauti namna ya kushika kamera na mikorofoni.
Nachotaka kusema kwa leo suala la wanahabari wenye diploma na shahada tu ndiyo wafanye kazi hii hilo ni kosa kubwa. Kwa kuwa sasa wameshatufundisha kazi ndiyo tunawatupa? Hilo haliwezekani.