Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Wiki ya Huduna za Fedha kitaifa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, akimkabidhi Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, kitabu cha Mpango wa Taifa wa Elimu ya Fedha baada ya kuzinduliwa katika Maonesho hayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, akiweka saini katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, akizungumza katika banda la BoT kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa. Katikati ni Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Bernard Kibesse na Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Bi. Vicky Msina.
Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha BoT, Bw. Ephraim Madembwe, akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, kuhusu namna ya kuwekeza katika Dhamana za Serikali.
Afisa Mkuu wa Benki BoT, Bi. Christina Nkya, akitoa elimu akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, kuhusu namna ya kutambua alama za usalama katika noti na namna bora ya utunzaji wa noti zetu.
Afisa Sheria wa BoT, Bw. Ramadhani Myonga akitoa elimu kwa mwananchi kuhusu Kanuni za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha kwenye banda la BoT kwenye Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa jijini Dar es Salaam.
********************************
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeandaa Kanuni za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha ambazo zinazingatiwa na watoa huduma za fedha wote nchini zikiwemo benki na makampuni ya simu, makampuni ya karadha, watoa huduma ndogo za fedha, na watoa huduma za malipo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Bernard Kibesse, amesema kuwa kanuni hizo zinalenga kuhakikisha uwazi na uwepo wa mfumo wa upokeaji na utatuzi wa malalamiko ya wateja pale wanapokuwa hawajaridhishwa na huduma iliyotolewa.
“Benki Kuu imeanzisha dawati la kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayohusu huduma za kifedha wanazopata kutoka katika benki na taasisi za fedha”, alisema Dkt. Kibesse.
Naibu Gavana aliongeza kuwa kuongezeka kwa uelewa wa masuala ya fedha katika jamii ya Watanzania kutawezesha wananchi wengi zaidi kutumia huduma za fedha katika namna inayoleta tija na kupunguza vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa vikifanywa na watoa huduma za fedha wasiojali maslahi ya watumiaji wa huduma hizo.
“Benki Kuu inahamasisha wadau husika kufikiria uwezekano wa kuanzisha somo la elimu ya fedha kwenye mitaala yetu na kulifundisha katika ngazi zote ili kuweza kuongeza uelewa, uwezo, ujuzi pamoja na kubadili mitazamo ya watoto tangu wakiwa wadogo”, aliongeza Dkt. Kibesse.
Aidha, Dkt. Kibesse alisema kuwa BoT inashiriki Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa lengo la kutoa elimu kwenye maeneo ya kipaumbele kama usimamizi wa benki na taasisi za fedha, Mfuko wa Bima ya Amana, dhamana za serikali pamoja na usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa.
BoT, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya teknologia katika kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinatolewa kwa ufanisi na gharama nafuu kwa mtumiaji.
Maonesho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu “Boresha Maisha kupitia Elimu ya Fedha” yamefunguliwa rasmi leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali.
Maonesho hayo ya kwanza na ya aina yake, yanashirikisha Wizara za Fedha na Mipango na taasisi mbalimbali za fedha za umma na binafsi kwa lengo la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.