Mwenyekiti wa bodi ya wahasibu wanawake Tanzania (TAWCA) Dokta CPA Neema Kiure akizungumza na wanavyuo wa chuo Cha uhasibu Arusha leo.(Happy Lazaro)
Mkuu wa chuo Cha uhasibu Arusha ,Profesa Eliamani Sedoyeka akizungumza na wanavyuo chuoni hapo katika siku ya uhasibu duniani .(Happy Lazaro)
Wanavyuo wa chuo cha uhasibu Arusha pamoja na wafanyakazi wa chuo hicho wakisikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika siku ya uhasibu duniani (Happy Lazaro)
**************************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Wanavyuo katika chuo cha uhasibu Arusha(IAA)wametakiwa kuongeza bidii katika masomo yao huku wakitumia ujuzi na uzoefu watakaoupata chuoni hapo kuweza kujiajiri katika fani ya uhasibu.
Hayo yamesemwa leo chuoni hapo na Mwenyekiti wa bodi ya wahasibu wanawake Tanzania (TAWCA) ,Dokta CPA Neema Kiure wakati akizungumza na wanavyuo hao katika siku ya uhasibu duniani ambayo hufanyika novemba 10 kila mwaka duniani.
Amesema kuwa, taaluma ya uhasibu ni pana sana na inamwezesha mtu yeyote kuweza kupata ajira, kikubwa ni kuhakikisha wanaongeza juhudi katika ujuzi na uzoefu walioupata chuoni hapo kwani ndio nyenzo zitakazowawezesha kuweza kujikwamua kiuchumi.
Dokta Neema amesema kuwa,endapo wataitumia taaluma hiyo vizuri kulingana na walivyofundishwa wataweza kufika mbali sana na kuweza kuwa mfano wa kuigwa kwani taaluma hiyo ni muhimu Sana kwa jamii inayotuzunguka kwani wanatutegemea kwa kiasi kikubwa.
“Nawaombeni sana wanavyuo msome kwa bidii kwani hata mimi nilisomea hapa na nimefika mbali Sana kupitia chuo hiki,hivyo mhakikishe mnakitumia vizuri msifanye mchezo muitumie elimu hiyo kuleta mabadiliko katika jamii inayowazunguka huku mkisaidia na vijana wenzenu pia.”amesema Dokta Neema .
Naye Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha,Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kuwa, chuo kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali kwa wanafunzi hao lengo likiwa ni kuwaandaa kuweza kupata ujuzi mbalimbali na kuweza kujiajiri kupitia fani ya uhasibu na kujikwamua kiuchumi.
Amesema kuwa,chuo hicho kimeweza kuongeza kozi ya maswala ya bima huku kikiendelea kuongeza kozi mbalimbali kila mwaka kulingana na uhitaji uliopo lengo likiwa ni kuwasaidia wanavyuo hao kuweza kupata ajira kwa urahisi huku wakiangalia mahitaji ya soko la ajira.
“Fani ya uhasibu ni ya muhimu Sana na mkae mkijua kuwa mhasibu akiyumba na Taasisi yake imeyumba ,na hivyo hivyo mhasibu akisimama na Taasisi yake pia imesimama na kwa Sasa mjione nyie ni wahasibu tayari na msikubali mtu yeyote awatoe kwenye malengo yenu mliyojiwekea .”amesema Profesa Sedoyeka.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo taaluma,utafiti na ushauri,Profesa Epafra Manamba amewataka wanavyuo hao kuzingatia masomo na kuhakikisha wanatoa mchango mkubwa katika kutumikia nchi yao huku wakiwa waadilifu na kuonyesha uzalendo katika Taifa kwa ujumla.
Naye Makamu wa Rais serikali ya wanafunzi chuoni hapo,Evitha Mutayoba amesema kuwa,anashukuru chuo hicho kwa namna ambavyo wamewaandaa vyema kuweza kuwa wahasibu wazuri na wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kwa namna ambavyo wanaandaliwa vyema chuoni hapo .
“Kwa kweli tunashukuru Sana kusherehekea siku ya uhasibu duniani ambayo inaleta chachu kubwa kwetu na kwa jamii kwa ujumla kuweza kutambua na kuona mchango wetu kama wahasibu katika kuinua uchumi wa nchi na Taifa kwa ujumla na tunaahidi kuifanyia kazi taaluma hii kwa kuleta mabadiliko kwa uzoefu na ujuzi tutakaoupata.”amesema.