Mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) umefanyika kwa njia ya mtandao leo tarehe 09 Novemba 2021 ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo” uliofanyika tarehe 06 Novemba 2021.
Mkutano huo ambao umeratibiwa na kuongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka umepokea mapendekezo ya miradi 12 iliyowasilishwa na Watanzania hao ambao ni Bw. Hassan Ng’anzo wa Norway, Dkt. Swabury Alawi wa Ujerumani na Bw. Patrick Dyauli wa Uingereza.
Wakiwasilisha mapendekezo ya miradi hiyo ambayo imejikita kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za Afya, Mazingira, Nishati, Madini, Ujenzi na Uchukuzi, Watanzania hao ambao pia ni wamiliki wa Kampuni za ANICO, ESSB na SE Holdings, wameiomba Serikali kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili kuwezesha miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji wa uhakika, kuja nchini kwani ina manufaa makubwa kiuchumi na itatengeza ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Balozi Rutageruka amewashukuru na kuwapongeza Watanzania hao kwa hatua hiyo ya kizalendo ya kuwa tayari kuja kuwekeza nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano watakaohitaji ili kufanikisha lengo hilo. Kadhalika, amewahimiza Diaspora wengine kujitokeza kwa wingi kuja kuwekeza au kuleta wawekezaji na wafanyabiashara wenye tija nchini.
Mkutano huo pia umewashirikisha wadau muhimu zaidi ya 20 kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. John Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahamoud Thabit Kombo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diapora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago, Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Sweden na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Wadau wengine walioshiriki ni kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, TIC, ZIPA na TANTRADE.
Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akichangia jambo wakati wa Mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 09 Novemba 2021. Kulia anayesikiliza ni Bw. Hassan Ng’anzo, Mtanzania anayeishi Norway ambaye aliwasilisha mapendekezo ya miradi ambayo wapo tayari kuja kuwekeza nchini. Miradi hiyo imejikita katika sekta mbalimbali kama vile afya, nishati, madini, mawasiliano na ujenzi na uchukuzi
Balozi Rutageruka akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi wakati akizungumza kwenye mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)
Balozi Rutageruka akimsikiliza Dkt. Swabury Alawi, Mtanzania anayeishi Ujerumani wakati wa mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)
Balozi Rutageruka akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diapora cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)
Mkutano ukiendelea huku Maafisa kutoka Idara ya Diplomasia ya Uchumi, Bw. Magabilo Murobi (kulia) na Bw. Herman Berege (kushoto) wakinukuu masuala muhimu yanayojadiliwa.