**********************
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOM.
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeee na Watoto yaendelea kusogeza zaidi huduma za kibigwa karibu Zaidi na Waanchi kwa kuanzisha Huduma za kusafisha damu (Dialysis) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Mtoto Dkt. Vivian Wonanji wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu upatikanaji wa huduma za kusafisha damu “dialysis” katika hospitali za rufaa za mikoa nchini Jijini Dodoma.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kusogeza huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi kwa kuanzisha huduma za kusafisha damu (Dialysis) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa.”Amesema Dkt. Wonanji.
Amesema kuwa, Mpango huu unatarajiwa kuanzishwa katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na baadhi ya hospitali za Halmashauri lengo ni kufikisha utoaji huduma karibu Zaidi na Wananchi na kwa gharama nafuu.
Aliendelea kusema kuwa, utekelezaji wa mpango huu, utafanyika kwa awamu, ambapo awamu ya Kwanza ilianza Mwezi Januari 2021 ikihusisha hospitali 7 za Rufaa za Mikoa ya Bombo (Tanga), Maweni (Kigoma), Musoma (Mara), Ligula (Mtwara), Mount Meru (Arusha), Bukoba (Kagera), na Iringa.
Aidha, Dkt. Wonanji amesema, awamu ya pili ambayo inatarajia kuanza mwezi huu wa Novemba, 2021 itazihusisha Hospitali 16 zikiwemo Hospitali 10 za Rufaa za Mkoa (Tumbi, Mwananyamala, Temeke, Amana, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Mawenzi, Mbeya na Songea), Hospitali 2 za Kanda (Chato na Uhuru) na Hospitali za Kimkakati (Mnazi Mmoja, Kigamboni, Palestina Sinza na AICC).
Hata hivyo Dkt. Wonanji ameweka wazi kuwa, awamu ya tatu itajumuisha Hospitali 11 za Rufaa za Mikoa ambazo ni (Njombe, Songwe, Lindi, Katavi, Rukwa, Singida, Tabora, Manyara, Shinyanga, Geita na Simiyu) na Hospitali ya Kanda ya Kusini, Mtwara.
Amebainisha kuwa, hadi kufikia Novemba 2021, Hospitali 6 za Rufaa za Mikoa tayari zimeshaanza kutoa Huduma ya Dialysis na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa itaaanza kutoa huduma hizi mara wakikamilisha mafunzo kwa watumishi.
“Hadi kufikia Novemba 2021, Hospitali 6 za Rufaa za Mikoa (Tanga, Kigoma, Mara, Mtwara, Arusha na Kagera) zimeshaanza kutoa Huduma ya Dialysis na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa itaaanza kutoa Huduma hizi mara wakikamilisha Mafunzo kwa watumishi.” Amesema.
Mbali na hayo ameweka wazi kuwa, mashine zilizowekwa katika hospitali hizi zina uwezo wa kufanya sessions 20 mpaka 30 Kwa siku. Huku akisisitiza kuwa, Mpaka kufikia sasa Hospitali hizo zimeweza kutoa jumla ya vipindi (sessions) 1,167 za kusafisha damu katika muda wa miezi 8; huku, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ikiongoza kwa kutoa vipindi 1,134 kuanzia mwezi Januari mwaka huu mpaka Agosti ambayo ilikuwa Hospitali ya kwanza kuanzisha Huduma hii katika ngazi ya Mkoa.
Pia, amesema kuwa, utekelezaji wa Awamu ya pili umeanza kwa ukarabati wa maeneo stahiki kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa, ambapo Bohari ya Dawa (MSD) itasambaza mashine za Dialysis165 na vitendanishi vyake, na timu ya wataalamu 16 kwa kila hospitali wanatarajiwa kuanza Mafunzo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Chuo Kikuu Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Bugando – Mwanza, Hospitali ya Mt. Meru – Arusha na Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Hata hivyo, ameeleza matarajio ya Serikali kuwa, Huduma kwenye hospitali 8 za awamu hii zitaanza mwishoni mwezi Desemba mwaka huu na kufikia mwishoni mwa mwezi Januari utekelezaji wa awamu ya pili utakuwa umekamilika. Aidha utekelezaji wa awamu ya tatu utaanza mwezi Machi na kutarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni 2022.
Ameeleza, Awamu ya Pili ya utekelezaji wa mpango wa huduma hii utaigharimu Serikali shs bilioni 6.5 ambayo ni gharama ya chini ukilinganisha na uwekezaji wa awamu ya kwanza.
Amesema, changamoto kubwa ya Huduma hii imekuwa bei ya Huduma kwani kwa sasa kipindi kimoja cha dialysis hugharimu kati ya Tshs 240,000 mpaka 300,000 na mgonjwa anahitaji vipindi vitatu yaani vipindi 12 kwa mwezi sawa na gharama ya kati ya Tsh 2,880,000 mpaka 3,600,000 kwa mwezi.
Dkt. Wonanji amesema kuwa, tayari MSD imechukua hatua ya kuwatafuta watengezaji wa mashine ili kuondoa gharama za ziada hali iliyosaidia kushuka kwa gharama mpaka shs 100,000 kwa kipindi kimoja cha Dialysis sawa na Tsh 1,200,000 kwa mwezi na shs milioni 14,400,000 kwa mwaka hali itayosaidia kuipunguzia mzigo wa gharama ya Huduma ya Dialysis kwa wananchi, NHIF na Serikali kwa ujumla.
Serikali imejipanga kuleta mabadiliko makubwa kwenye Huduma ya kusafisha damu Nchini na Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika kuwa na gharama za bei nafuu hivyo tunaomba wananchi waendelee kupata Huduma kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa kadri tutakavyokuwa tunasogeza Huduma ya Dialysis karibu, amesisitiza