Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwahemu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Mwananchi wa Kijiji cha Chenene Bw. Amiri Mamba akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimkabidhi fedha mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Chenene kwa ajili ya kununua mpira wa miguu utakaowawezesha wanafunzi wa shule hiyo kufanya mazoezi ya kujenga afya zao ili waweze kushiriki masomo kikamilifu.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Chamwino Bw. Sehewa Msagatwa akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya Kijiji cha Kwahemu kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
*******************************
Na. Veronica Mwafisi-Chamwino
Tarehe 09 Novemba, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inagusa maisha ya kila Mtanzania kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unaziwezesha kaya zote maskini nchini kupata ruzuku inayozisaidia kuboresha maisha yao.
Mhe. Ndejembi amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chenene na Kwahemu, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) wilayani Chamwino.
Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, TASAF inamgusa kila mtu kwani kama kaya yako haipo basi ya jirani yako inanufaika, na kama binafsi haunufaiki basi ndugu yako yeyote ananufaika.
“Kama kaya yako hainufaiki, ya ndugu yako inanufaika na kama wewe binafsi haunufaiki basi Shangazi, Mjomba, Babu au Bibi ananufaika na TASAF,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Katika kuhakikisha fedha za mradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali, Mhe. Ndejembi amewaasa wanufaika wa TASAF kutumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao badala ya anasa.
“Serikali haijamkataza mnufaika wa TASAF kunywa pombe, lakini ahakikishe hanywi pombe kwa kutumia fedha zinazotolewa na Serikali kupitia TASAF kwani fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuboresha maisha ya kaya maskini na si kustarehe,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza kuwa TASAF ni mradi kama ilivyo miradi mingine, kuna siku utafikia ukomo hivyo walengwa wanapaswa kuutumia vema ili wasijute kwa kutotumia fedha hizo kuboresha maisha yao.
Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuweka mkakati wa kuboresha maisha yao kupitia TASAF kwani haoni sababu ya wanaonufaika kutumia fedha hizo tofauti na malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Mhe. Ndejembi amesema, Serikali inatarajia baada ya mradi wa TASAF kufikia tamati, wanufaika wa TASAF wamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kuku ikiwa ni pamoja na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora za kuishi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Chenene na Kwahemu vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.