********************************
Wakazi wa Kata ya Magata Karutanga, wilaya ya Muleba, mkoa wa Kagera wamehimizwa kuongeza kasi ya ujenzi ya miundombinu ya madarasa kwa fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Serikali.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya Sekondari Kishoju ambapo amemhimiza Mkuu wa shule hiyo pamoja na mafundi wanaojenga vyumba hivyo vya madarasa kuongeza kasi na jitihada ili kuhakikisha kufikia tarehe 30.11.2021 wawe wamemaliza ujenzi huo.
“Tumezoea kila mwaka kukimbizana na ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wapate kuingia darasani kwa wakati. Kutokana na changamoto hiyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya madarasa, hivyo nawasisitiza kila kata iliyopewa fedha za ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine kuhakikisha tunajenga na kukamilisha kwa wakati kama maagizo yaliyotolewa yanavyoelekeza,” ameeleza Mhe. Nguvila.
Sambamba na hilo amewasisitiza wananchi wa kijiji cha Kasheno kujitokeza na kujitolea kujenga zahanati ya kijiji na kuanza kufikiria kuwa na kituo cha afya cha kata yao ili kuondokana na tatizo la upatikanaji wa huduma za afya kiurahisi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kasheno, Mhe. Nguvila amemuagiza Diwani wa kata hiyo kukaa na Kamati yake ya Maendeleo ya Kata (WDC) kuangalia sehemu ambapo watajenga kituo cha afya na kuwashauri kujenga zahanati kwa kila kijiji na mpango wa kujenga zahanati ijengwe na kijiji husika na Serikali itawaongezea nguvu.
“Anzeni nyinyi kujenga, mpendekeze kama ni hapa au Ruhanga mtapendekeza sehemu ya kujenga zahanati, mkianza Serikali itawasaidia hata mkianza kwa kuchimba msingi na mimi mwenyewe nitakuja kuwaunga mkono,” amesema Mhe. Nguvila
Aidha, Mhe. Nguvila amewahimiza wananchi wa Kata hiyo kutowafundisha watoto wao tabia ya kufanya vibaya katika mitihani na kuwasisitiza kuwa wakiwazuia watoto kusoma maisha yao yatakuwa si mazuri, wengine watakuwa majambazi na wanaweza kusababisha kuja kulaumiwa na watoto wao baadae kwa kutowapeleka shule.
Pamoja na hayo Mhe. Nguvila amewasihi viongozi wa Kata na Vijiji kuhakikisha wanapambana na suala la uvuvi haramu ambapo amewasisitiza kuhakikisha wanasalimisha makokoro na zana haramu zote kwa lengo la kuweza kupambana na uvuvi haramu.
“Mimi na kikosi cha kudhibiti uvuvi haramu tukikamata mtu unakwenda mahakamani, mahakama itakuhukumu kulingana na kosa lako ama kutozwa faini ama kufungwa gerezani kwa sababu azimio letu ni kuweka uvuvi endelevu na kukomesha uvuvi haramu”, amesisitiza na kuonya Mhe. Nguvila.
Afisa Kilimo Ndg. Diocles Lwekamwa amewasisitiza wananchi wa kata hiyo kulima mazao ya muda mfupi kama mihogo na viazi kwa sababu maeneo mengi mvua hazitoshelezi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Naye Afisa Lishe Ndg. Tigelelwa Robinson ametoa elimu kwa wananchi wa kata hiyo hasa akina mama kwa kuwambia kuwa wakati wa ujauzito wahakikishe wanameza dawa za kuzuia utapiamlo kwa watoto walioko tumboni kwani kumekuwa na changamoto ya wakina mama wajawazito kutozitumia dawa hizo kikamilifu kwa kudai kuwa wanapata kichefuchefu na kuongeza kuwa pindi wanapozaa watoto wenye utapiamlo wasisite kuwapeleka kwenye vituo vya afya kupatiwa huduma.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Ndg. Barnabas Richard amemuagiza mama aliyetelekezwa na mume wake na kumuachia familia ya watoto wanne kufika ofisi ya Ustawi wa Jamii Muleba kwa ajili ya kushughulikiwa suala lake.
Mwisho Mhe. Nguvila amemuagiza Afisa Ustawi wa Jamii kutafuta mbinu mbadala ili huyo mwanaume aliyeitelekeza familia yake afuatwe aliko ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.