Afisa mwandamizi kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma,Paul Makelele akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha(Happy Lazaro).
Afisa mwandamizi kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma ,Paul Makelele akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo(Happy Lazaro)
*****************************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Wadau kutoka nchi ya Tanzania na Kenya wamekutana jijini Arusha kwa ajili ya kufanya majadiliano ya mikataba ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa mwandamizi kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dodoma,Paul Makelele wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Makelele amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kutokana na maelekezo ya mkutano wa ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliofanyika nchini Kenya , Nairobi Kati ya tarehe 20 hadi 24 agosti ,2021.
“katika mkutano huo ilielekezwa kwamba Kuna mikataba ambayo haijakamilika na haijasainiwa Kati ya Tanzania na Kenya ,hivyo ilielekezwa kuwa timu za pande zote mbili za wataalamu kutoka Tanzania na Kenya wakutane Tanzania ili kuja kukamilisha majadiliano ya mikataba hiyo na ikiwezekana isainiwe kwa miezi michache ijayo.”amesema Makelele.
Amesema kuwa, mikataba inayojadiliwa ni makubaliano kuhusu maswala ya uhamiaji,mkataba kuhusu maswala ya kupeana wahalifu,mkataba kuhusu maswala ya kusaidiana kwenye makosa ya jinai,mkataba kuhusu kubadilishana wafungwa kwani kuna watanzania ambao wamefungwa nchini Kenya na kuna wakenya ambao wamefungwa nchini Tanzania, hivyo tukikamilisha majadiliano hayo tutaomba watanzania kuja kutumikia kifungo nchini kwetu na wakenya kuweza kutumikia kifungo nchini kwao.
Ametaja makubaliano mengine kuwa ni kuhusu maswala ya magereza na wafungwa na makubaliano kuhusu maswala ya uwekezaji.
Ameongeza kuwa, majadiliano hayo yatadumu kwa siku tano na yatakamilisha makubaliano na mikataba hiyo ili iweze kusainiwa na pengine kwa miezi michache inayokuja.
Makelele amesema kuwa,mkutano huo ni kwa ngazi ya wataalamu kutoka uhamiaji ,magereza,wizara ya katiba na sheria,ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali,wizara ya mambo ya ndani ya nchi , viwanda na biashara,wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makelele ameongeza kuwa,mkutano huo pia umehudhuriwa na Balozi waTanzania nchini Kenya John Simbachawene na Balozi wa Kenya nchini Tanzania , Dan Kazungu.
Amesema kuwa, baada ya mkutano huo utaimarisha zaidi ushirikiano wa nchi zote mbili hasa katika maeneo hayo yote muhimu .