*****************************
Na Silvia Mchuruza,
Muleba,Kagera.
Wananchi wa Kijiji cha Katembe, Kata ya Nyakabango, Wilaya ya Muleba wameanza kunufaika kwa kufunguliwa kwa soko la samaki na dagaa lililopo mwalo wa Katembe-Magarini ambapo kupitia soko hilo limewainua hali zao za kiuchumi kwa kuwawezesha kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali kama kuuza bidhaa za madukani, ubebaji wa mizigo na shughuli za mama lishe.
Akiendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kulitumia soko hilo la Katembe-Magarini kwa ajili kusafirisha samaki na dagaa kwenda sehemu mbalimbali nje na ndani ya nchi, Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amesema kuwa ataendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha biashara zao katika mazingira bora na salama ambayo yatawawezesha wao na Serikali kupata faida.
“Hapa hatuna vikwazo vyovyote kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kwenda nje na wafanyabiashara wa ndani gharama ni ndogo ukilinganisha na gharama ambazo zinatozwa kwenye mialo mingine. Tumewapunguza tozo ili wafanyabiashara hawa waweze kufanya biashara kwa urahisi na wapate faida na Serikali pia ipate faida,” amesema Mhe. Nguvila.
Aidha, ameendelea kueleza kuwa baada ya soko kufunguliwa mapato ya Serikali kuu na Halmashauri yamepanda kwa sababu kabla ya kufunguliwa kwa soko hilo wafanyabiashara na wavuvi walikuwa wanatorosha mizigo kupitia mialo mingine kwenda nje ya wilaya ya Muleba bila kulipia mapato ya Halmshauri lakini baada ya kufunguliwa kwa soko hilo mapato ya Halmashauri yameongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.
Kuhusiana na daraja amesema kuwa wapo kwenye mkakati wa kulipandisha juu urefu wa mita mbili ili kuwawezesha watumiaji kuendelea kulitumia daraja hilo bila changamoto ya kuhofia maji kujaa juu ya daraja.
Kwa upande wake Afisa uvuvi wa wilaya Ndg. Wilfred Tibendelana ameeleza kuwa kwa sasa wananchi wa eneo la mwalo wa Katembe tayari wameshaanza kunufaika na soko la dagaa na samaki na wakati huohuo kuwezesha Serikali kuu na Halmashauri kupata mapato. Pia ameendelea kuwasisitiza wafanyabiashara wote waliopo ndani na nje ya wilaya ya Muleba kuendelea kulitumia soko la hilo la Katembe-Magarini kwani tozo zake ni ndogo ukilinganisha na maeneo mengine.
Msimamizi mkuu wa Bandari ya Katembe-Magarini Ndg. Sande Ruben Mtambo ametoa takwimu na kusema kuwa tangu mizigo ya dagaa ianze kushushwa kupitia bandari ya Katembe-Magarini mpaka sasa zimeshushwa tani 13,033.95 na mapato yameongezeka kwa wastani wa kutoka milioni 13 hadi kufikia milioni 16 kwa mwezi mmoja.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji Ndg. Obadia Mtesigwa Mafuru amesema kuwa mwanzoni kabla ya soko kufunguliwa wananchi wa eneo hilo walikuwa na shida ya bidhaa zao kutokuwa na mzunguko wa kibiashara lakini baada ya soko kufunguliwa tayari wananchi wananufaika vizuri na soko la hilo, hivyo anaendelea kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuja kununua dagaa katika soko hilo.