NA BALTAZAR MASHAKA, KAHAMA
SERIKALI ya Awamu ya Sita imeshauriwa kuufufua Mpango wa Kilimo Kwanza na kuufanya endelevu ili kuleta tija kwenye mnyororo wa thamani na kuwakomboa wakulima nchini.
Ushauri huo ulitolewa wilayani Kahama na Mkurugenzi wa Nyanembe Agriculture Farm,Khamisi Mgeja,wakati akizungumza na waandishi wa habari,walipomtembelea jana shambani kwake katika Kijiji cha Nyanembe,kujionea shughuli anazofanya za kilimo na mradi wa uchimbaji wa mabwawa ya maji ya kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia zana duni zisizo na ubora.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inafanya jitihada kubwa za kuwasaidia wakulima na kuinua sekta ya kilimo,hivyo haina budi kuhuisha Mpango wa Kilimo Kwanza na kuufanya endelevu kwa kuunganishwa na mpango wa sasa ili uwe dira ya taifa kwenye sekta hiyo.
“Tunafahamu kilimo ni uti wa mgongo na uchumi wa taifa letu unategemea sekta hiyo, ni eneo namba moja linalotoa ajira kubwa kwa Watanzania nchini,hata sera ya Tanzania ya viwanda bila kuwekeza kwenye kilimo kwa kiwango cha juu, mafanikio na tija yake yatakosa matokeo mazuri,”alisema Mgeja.
Aliomba kutokana na umuhimu wa kilimo ni vyema kikapewa kipaumbele na msukumo mkubwa kama ilivyofanyika kwenye miradi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, hilo likifanyika litawawezesha wakulima kunufaika na kilimo.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema ni muhimu taifa likawekeza nguvu kwenye kilimo kwa kuwa na mpango kabambe wa kufa na kupona,kuhakikisha kinawakomboa wananchi kutoka kwenye umasikini wa kipato kwa kuzalisha mazao ya biashara yatakayoongeza pato la taifa na kujitosheleza kwa chakula.
Mgeja ambaye kwa sasa anajishugulisha na kilimo pamoja na ufugaji baada ya kupumzika siasa,alionyesha masikitiko makubwa kuwa mipango mizuri yenye tija kwa nchi inapotelekezwa inatia uchungu na kutolea mfano kilimo kwanza ulioasisiwa na Serikali ya Awamu ya Nne kuwa ulihujumiwa na watu wachache wenye maslahi ya ghiliba wezi, mafisadi na waliokosa uadilifu.
Alidai Mpango wa Kilimo Kwanza ulihujumiwa na watu walafi wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka haraka,waliolenga kuwaumiza wakulima na kuwakosesha matumaini kwenye serikali yao na hivyo kusababisha kipoteze mwelekeo.
“Tunafahamu mawakala waliopewa na serikali ya awamu ya nne kazi ya kusambaza pembejeo,viuadudu na zana za kilimo kwa nia njema ili kuwasaidia wakulima,baadhi ya watalaamu na watumishi wa umma walikosa uaminifu kwa kupiga deal,hujuma zilisababisha hasara kwa wakulima na serikali,kwa sababu ya wezi hao na kukosa usimamizi madhubuti wa kilimo kwanza,”alisema Mgeja.
Mkurugenzi huyo wa Nyanembe Agriculture akiwa shambani kwake akichimba mabwawa ya umwagiliaji,alitahadharisha asijitokeze mtu,kikundi chochote ama kampuni kuthubutu kuhujumu mipango mizuri ya serikali inayolenga kuwasaidia na kuwakomboa wakulima kikiwemo kilimo.
Alishauri itungwe sheria dhidi ya watakaojihusisha na hujuma ya mipango ya serikali hasa wizi na ubadhirifu kwenye pembejeo,viuadudu na zana zote za kilimo,wafunguliwe kesi za uhujumu uchumi,wakithibitika wafungwe kifungo kisichopungua miaka 30 jela na kucharazwa viboko hadharani.
“Tuna imani na Rais Samia, serikali yake hasa utendaji wa Waziri Mkuu (Majaliwa Kassim), Waziri wa Kilimo, Profesa Aldof Mkenda na Naibu Waziri wake, Hussein Bashe,wanastahili pongezi kwa kazi nzuri wanaoifanya usiku na mchana ya kuhakikisha kilimo kinainuka,kinaimarika na kuleta tija na manufaa kwa wakulima,”alisema Mgeja.
Pia alimpongeza Rais Samia kwa kutoa mabilioni ya fedha kununua mahindi ya wakulima kwa bei yenye tija baada ya kukosa soko la uhakika na kuwaondoa kwenye mikono ya walanguzi na wanyonyaji, kitendo ambacho hakijafanywa na serikali kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, ameonyesha dhamira njema kwa kuwasaidia wananchi wake na wakulima kuinua vipato vyao,hivyo wananchi waendelee kumuunga mkono na serikali yake kwa kuchapa kazi na ana imani atawavusha na kuwafikisha mahali pazuri kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania.ssss