Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC (katikati) akiwa katika moja la jengo la muda lililojengwa maeneo ya fukwe za Coco Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC (wa tatu kushoto) akitoa maelekezo kwa wakaguzi wa mazingira kutoka NEMC baada ya kuwasli fukwe za Coco.
*************************
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa maeneo ya fukwe au vyanzo vya maji ni maeneo nyeti kimazingira kwa sababu ni maeneo ambayo yanategemewa na viumbe wa Baharini na Jamii inavitegemea.
Ameyasema hayo alipofanya ziara pamoja na wakaguzi wa mazingira kutoka NEMC katika maeneo ya fukwe za Coco jijini Dar es Salaam. Lengo la ziara hiyo ni kwa ajili ya ukaguzi wa mazingira katika eneo hilo.
Aidha, Dkt. Gwamaka ameeleza kuwa ziara hiyo katika maeneo ya Fukwe za Coco ni kutokana na ujenzi au maendeleo yanayofanyika katika eneo hilo kuangalia kama yamezingatia Sheria ya Mazingira 2004 ambayo inasema maendelezo yoyote ambayo ni ya kudumu au ambayo yanaweza kuleta athari zozote za kimazingira basi yafanyiwe Tathmini ya Athari ya Mazingira.
ameendelea kusema “mazingira ya fukwe za Coco kwa sasa yanaridhisha kutokana na ujenzi wa majengo ya muda yanayovutia yaliyojengwa maeneo hayo ambayo yanatoa nafasi kwa wajasiliamali wenye kipato cha chini kujipatia fedha za kujikimu pamoja na watu kupata sehemu nzuri ya kupumzika na kuweza kula. Pia nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na uongozi wake wote kwa jitihada wanazofanya kuwatengea maeneo wajasiliamali wadogo na vilvile kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa utaratibu maalum kama ambavyo ujenzi wa vibanda visivyo vya kudumu unavyoendelea katika fukwe za Coco” Dkt.Gwamaka
Dkt. Gwamaka amesema kuwa watashirikiana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Manispaa ya Kinondoni ilikuona namna gani wataboresha maeneo hayo ili kukabiliana na changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe unaosababishwa na Mabadiliko ya Tabianchi kwa hiyo mahali hapa panatakiwa kufanyiwa maboresho kwa kuweka mawe ambayo yatasaidia maeneo haya yawe endelevu pamoja na kuboresha miundombinu ya maji taka na maegesho ya magari
Amemaliza kwa kusema kuwa jambo kubwa la kuzingatia maeneo haya ni kuongeza idadi ya vyoo kwani kutokana na muonekano mzuri wa maeneo hayo basi watu wengi watavutiwa kuja hapa. NEMC tutakuwa bega kwa bega na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha mahali hapa panakuwa salama wakati wote ili eneo hili liwe eneo ambalo wananchi wa kawaida wanaendelea kufaidi matunda ya uhuru wa Nchi, na liwe eneo la mfano kwa wajasiriamali wadogo kwa nchi nzima ya Tanzania.