Balozi Rutagaruka ametoa wito huo hivi karibuni wakati wa Mdahalo wa
Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa
katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo” uliofanyika kwa njia ya mtandao na
kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wabunge, Mabalozi na Wanadiaspora. Akizungumza kwenye Mdahalo huo
akiwa jijini Dodoma, Balozi Rutagerua amesema kuwa, upo umuhimu mkubwa kwa Tanzania
kuendelea kuimarisha mahusiano yake na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda
na kimataifa ili inufaike kiuchumi kupitia fursa lukuki zilizopo nchini kama
vivutio vya Utalii, fursa za Uwekezaji na Biashara pamoja na kuhakikisha wadau
wote zikiwemo Taasisi za Umma na
Binafsi, Mabalozi na Wananchi kwa ujumla wanashiriki kikamilifu katika kutekeleza
mikakati mbalimbali iliyopo ili kufikia
malengo kusudiwa kupitia Diplomasia ya Uchumi. Ameongeza kusema kuwa, tayari
mafanikio mengi yamepatikana kupitia utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi
ikiwemo kuimarika kwa Sekta za Uchumi ambapo tayari mikataba kadhaa ya manufaa kwa
nchi imesainiwa ukiwemo ule wa Serikali ya Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kampuni ya
Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP) itakayohusika na Ujenzi wa Mradi wa
Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga. Mafanikio
mengine ni kuondolewa kwa vikwazo 46 kati ya 64 vya muda mrefu visivyo vya kiforodha
kati ya Tanzania na Kenya. Vikwazo hivi vimeondolewa kufuatia ziara ya Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya mwezi
Mei 2021. Kadhalika amesema kuwa, Tanzania
imeimarisha ushiriki wake katika masuala ya kikanda na kimataifa na kwamba
mwezi Septemba 2021 Tanzania iliridhia Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la
Biashara Barani Afrika na kwamba kuridhiwa kwa mkataba huu kumeongeza ushawishi
wa Tanzania katika mtangamano wa Afrika na kuwa sehemu ya soko kubwa la Afrika
lenye idadi ya watu wapatao bilioni 1.3. Aliainisha maeneo mengine ya mafanikio
kuwa ni pamoja na kukua kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili na ufunguzi wa
Balozi na Konseli Kuu ambapo hadi sasa Tanazania inazo Balozi 44 na Konseli Kuu
6. Mbali na mafanikio hayo, Balozi Rutageruka amesema Serikali itaendelea
kutekeleza kikamilifu mikakati iliyopo ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ikiwa
ni pamoja na kuvutia utalii, uwekezaji na biashara kwa kutumia maonesho na
makongamano; kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika Jumuiya za
Kikanda na Kimataifa; kutafuta fursa za masomo na ufadhili; kubadilishana ujuzi
katika nyanja mbalimbali kati ya Taasisi za Tanzania na Taasisi nyingine nje ya
nchi na kutumia Balozi za Tanzania katika kutangaza vivutio vya utalii na fursa
za uwekezaji na biashara zilizopo nchini. Kwa upande wake, Balozi wa
Tanzania nchini Korea ya Kusini, Mhe.
Togolani Mavura ambaye wakati wa mdahalo huo alizungumzia umuhimu wa Diplomasia
amesema ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kuwekeza kwenye Diplomasia hususan
kuimarisha ushirikiano na nchi zingine ili kuepusha migogoro ambayo husababisha
nchi kupoteza mwelekeo na badala ya kuokoa fedha kwa ajili ya huduma muhimu za
jamii kama maji, afya na umeme nchi zinajikuta zinawekeza kwenye masuala ya
migogoro na vita ambayo hugharimu fedha nyingi. Naye Naibu Mwakilishi wa Kudumu
wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mhe. Hoyce Temu amesema Tanzania
chini ya Utawala wa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea
kung’aa kimataifa na kwamba mashirika mbalimbali ya kimataifa yameonesha nia ya
kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake hususan kwenye agenda mbalimbali ikiwemo
ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030. Akichangia hoja wakati wa
mdahalo huo, Bi. Loveness Mamuya ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani amesema
Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) ipo tayari kushirikiana na
Serikali katika kuchangia maendeleo ya nchi na kutoa rai kwa Serikali
kuwashirikisha kikamilifu Diapora kwenye mipango mbalimbali ikiwemo kutafuta
wawekezaji na wafanyabiashara wa uhakika kutoka kwenye maeneo waliyopo. Mdahalo huo ambao umeandaliwa
na Taasisi ya Watch Tanzania na kuwashirikisha
wazungumzaji mbalimbali umeongozwa na Dkt. Hezron Makundi, Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Diplomasia ya Uchumi ni
Mkakati wa nchi kushirikiana na mataifa mengine, mashirika au taasisi za
kimataifa kujinufaisha kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji, utalii na teknolojia.
|