………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Arusha
Mashidano ya maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameanza Novemba 06, 2021 katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid na Ngarenaro Complex vya jijini Arusha yamepamba moto kwa michezo mbalimbali inayoendelea katika viunga vya jiji hilo.
Maadhimisho hayo yamezinduliwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul yamechagizwa na mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kwa wanaume, netiboli, mchezo wa kuvuta kamba, mpira wa wavu na mpira wa Mpira wa kikapu.
Mashindano hayo yamekuwa ni chachu ya kubadili mtindo wa maisha na kuboresha afya ya wananchi wa mkoa wa Arusha kufanya mazoezi ili kuendelea kulinda afya zao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hatua inayowasaidia kujikita zaidi katika shughuli zao za kila siku za maendeleo.
Katika mchezo wa mpira wa miguu timu za Manzese na Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru (TICD) zote za jijini humo zikitandaza soka safi katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid hadi dakika 90 za mchezo zilitoshana nguvu kwa sare ya 0-0 hatua iliyopelekea timu hizo kwenda hatua ya matuta ambapo timu ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru imeibuka kidedea kwa kuwafunga Manzese FC kwa jumla ya penalti 9-8.
Mchezo wa netiboli zilichezwa mechi mbili ambapo katika mchezo wa kwanza ulizihusisha timu za Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru (TICD) ambao wamecheza dhidi ya United Queens ya Sakina (33-21) na mchezo wa pili ukazihusisha timu za Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru (TICD) na Maasai Queen ambao nao matokeo yao yakawa (08-35).
Michezo mingine iliyochezwa ikiwa mwendelezo wa wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ni mpira wa kikapu uliozihusisha timu za Soweto na Spiders ambao nao walifungana kwa jumla ya magoli 65-63.
Mchezo wa mpira wa wavu nao haukuachwa nyuma katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambapo ilichezwa michezo mitatu na kuzihusisha timu za Pentagon ambao waliwashinda timu ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa seti (3-2), Arusha Champions waliwashinda timu ya Pentagon kwa seti (3-1) na mchezo wa tatu kwa upande wa wanaume ulizihusha timu Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ambao walifungwa na timu ya Arusha Champions kwa seti (1-3).
Kwa upande wa wanawake katika mchezo wa wavu, timu Pentagon walifungwa na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa seti (1-3).
Maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika kuanzia Novemba 06 hadi 13, 2021 yakiongozwa na kauli mbiu ya inayowasisitiza “Badili Mtindo wa Maisha, Boresha Afya” kwa lengo la kuitaka jamii ya watanzania na wadau wote kushirikiana katika kubadili mtindo wa maisha ili kuwa na afya bora na yenye kuleta tija kwa Taifa letu.