…………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Mafia
WANAFUNZI wa kisiwa cha Jibondo wilayani Mafia wanaohitaji elimu ya sekondari wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa shule ya sekondari ambapo wanalazimika kufuata elimu hiyo kwa kuvuka maji hadi Mafia .
Baadhi ya wazazi na walezi Jibondo waliiomba serikali wilaya kuharakisha upatikanaji wa shule ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ili kukomboa sekta ya elimu Jibondo.
Sophia Ally mkazi wa Jibondo alisema, tatizo la usafiri wa majini kila siku kwenda na kurudi linashusha ari ya kusoma kwa watoto wao ,”elimu Yao wanaipata kwa shida sana na hata wale wanaofaulu kuingia kidato cha tano na sita, kwa Mafia mwisho kidato cha nne hivyo wanafuata elimu hiyo Bara.
Mkuu wa wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo,akijibu kuhusiana na kero hiyo alisema serikali imeshatenga sh.bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Jibondo itakayojengwa ndani ya miezi sita.
Alisema kwasasa hatua ya kuvuta maji na kujenga msingi zimekamilika ,bali tatizo lililopo ni namna ya kusafirisha vifaa vya ujenzi kwa njia ya maji ikiwemo matofali na mchanga.
“Miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea ikiwa ni pamoja na shule hii ya sekondari Jibondo, tatizo ni suala la usafiri ndilo linalochelewesha hasa vifaa “
“Tumeshaongea na TEMESA na Jeshi ambalo limeahidi kushirikiana nao kusaidia namna ya kutatua changamoto hiyo”alifafanua Ntemo.
Ntemo alielezea , ujenzi unatarajiwa kuwa na vyumba 13 vya madarasa ,maabara 3,matundu ya vyoo 16,sehemu ya kulia chakula na nyumba za walimu.
Nae mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) Clement Kivegalo anaeleza, wamejipanga kutatua changamoto ya maji Mafia ikiwemo Jibondo,Kilindoni na kuahidi kuangalia namna ya kusogeza huduma ya maji kwenye shule hiyo.