Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akiwafafanulia wahifadhi kutoka Makumbusho ya Zanzibar (hawapo pichani) sura mpya ya Kijiji cha Makumbusho itakavyo kuwa.
Kushoto ni Mhifadhi Mwandamizi wa Makumbusho ya Zanzibar, Bw. Kheri Bakari, akimfafanulia jambo Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga (kulia)
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga na wahifadhi kutoka Makumbusho ya Zanzibar pamoja na wa Makumbusho ya Kijiji wakiingia kwenye nyumba ya Waswahili iliyopo Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga (kulia), kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Bw Mawazo Ramadhani pamoja na wahifadhi kutoka Makumbusho ya Zanzibar wakitembelea Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam
**************************
Na Sixmund J. Begashe
Makumbusho ya Taifa nchini imeanza mchakato wa ujenzi wa nyumba ya asili ya watu wa Zanzibar kama sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuboresha mashirikiano katika uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni na Idara ya Makumbusho na Malikale ya Zanzibar.
Akizungumza na wahifadhi kutoka Zanzibar, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini, Dkt Noel Lwoga amesema ni wakati sasa wa kuhakikisha Makumbusho ya Taifa kupitia Kijiji cha Makumbusho iliyopo Kijitonyama Dar es Salaam, inabeba sura ya utanzania kwa kuwa na nyumba ya asili ya Zanzibar.
“Sisi ni Tanzania, Kijiji cha Makumbusho kinahifadhi urithi wa utamaduni wetu. Uwepo wa nyumba sinazoakisi utamaduni wa Zanzibar utafanya Kijiji cha Makumbusho kama hifadhi ya utamaduni wa Mtanzania” alisema Dkt. Lwoga.
Dkt. Lwoga aliongeza kuwa hii inamaana kubwa hasa katika sekta ya utalii kwani itaongeza thamani ya Kijiji cha Makumbusho na kutoa fursa kwa watalii wanaotembelea Kijiji hicho kupata ladha ya maisha ya wakazi wa Zanzibar kabla hawaja fika katika visiwa hivyo, jambo litakalo wavutia watalii hao kwenda visiwani huko.
Naye Mhifadhi Mwandamizi wa Makumbusho ya Zanzibar, Bw. Kheri Bakari aliipongeza Makumbusho ya Taifa kwa hatua inayozichukuwa za kuimarisha mashirikiano na kwamba wao kama wataalam wamejipanga kushirikiana na Wataalam wa Bara kuhakikisha Nyumba zenye mahadhi ya utamaduni wa Zanzibar zinajengwa Kijiji cha Makumbusho.
“Makumbusho ya Taifa imepiga hatua kubwa sana hasa katika kuimarisha Mahusiano na sisi katika uhifadhi, ni kweli huwezi kuwa na Tanzania bila Zanzibar sisi tunaunga mkono uwamuzi huu na tutahakikisha azma hii inatimia haraka” alisema Bw Bakari.
Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Bw Mawazo Ramadhani amesema ofisi yake pamoja na wataalam wamejipanga vyema kuhakikisha azma ya Taasisi kuwa na makazi hayo inafanyika mapema ili kutoa fursa ya watalii hasa wandani kujifunza na kuburudika kupitia uhifadhi huo wa kiutamaduni.
Makumbusho ya Taifa imejiwekea mkakati mkubwa wa kukiboresha Kijiji cha Makumbusho kwa kujenga nyumba za asili kufuatana na ramani ya Tanzania ili kutoa nafasi kwa wageni mbalimbali kupata uwasilia wa makazi ya halisi ya makabila yaliyopo nchini.