Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu Serikali Bw. Emmanuel Tutuba akifungua Kikao Kazi kati ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa Vyombo vya habari mbalimbali nchini hivi karibuni Kikao hicho pamoja na mambo Kadhaa kilijadili kuhusu Sekta ya Fedha na Maadhimisho ya wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Kambarage Ofisi ya Hazina jijini Dodoma.
Kamishna Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja akitoa maelezo ya kikao kazi hicho kabla ya kufunguliwa hivi karibuni kati ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa Vyombo vya habari mbalimbali nchini, Kikao hicho pamoja na mambo Kadhaa kilijadili kuhusu Sekta ya Fedha na Maadhimisho ya wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Kambarage
******************
Tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la umaskini hapa nchini ikiwa wananchi wengi watakuwa na uelewa wa huduma za fedha na hilo ni jukumu letu hapa Wizarani tukishirikiana na wadau wa sekta hii*( Dr. Charles A. Mwamwaja- Kamishna Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha- Wizara ya Fedha na Mipango)
Kati ya tarehe 8 mpaka 14, Novemba, 2021 kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es alaam, kutakuwa na maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ambayo ni maadhimisho ya kwanza ya aina hii katika historia ya uendeshaji wa uchumi wetu. Ni tukio muhimu kwa uchumi wa watu linaloanzia Dar es alaam likiwa na matarajio lukuki ya kuwafikia wengi kila kona ya nchi kwenye siku za usoni.
Maadhimisho ya mwaka huu yana kauli mbiu isemayo; *Boresha Maisha kupitia Elimu ya Fedha*. Ni kupitia kauli mbiu hii, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Idara mbalimbali za Serikali, watafiti, wanahabari, wanataaluma, tasasisi za kiraia na wadau wengine wanalenga kuratibu zoezi la kuwapa uelewa wananchi wengi juu ya huduma za kifedha zilizopo nchini, aina za huduma na manufaa yake, maarifa ya kuzitumia huduma hizo na sababu zake. Miongoni mwa huduma zenyewe ni mikopo, huduma za bima, hatifungani, kuweka akiba,masoko ya fedha na usimamizi wa fedha binafsi miongoni mwa huduma nyingi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bwana Emmanuel Tutuba; Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni Moja ya mikakati ya kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ya Mwaka 2020/21-2029/30 unaolenga kuongeza uelewa wa masuala ya fedha kwa wananchi kufikia asilimia themanini (80%)ifikapo mwaka 2025.
KWA NINI KUSHIRIKI MAADHIMISHO HAYA?
Kwa kiwango cha Kitaifa, maadhimisho haya yatakufanya wewe mfanyabiashara, mjasiriamali, mtumishi wa umma, mfanyakazi kwenye sekta binafsi, mkulima, dereva, mfagiaji, mwendesha pikipiki au mwanahabari kuelewa huduma za kifedha kwenye uchumi wa Tanzania na hivyo kuweza kuzifikia katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Kwa mtu mmoja-mmoja, wiki hii ni muhimu wakati huu ambapo unamaliza mwaka na kujiandaa na mipango mingi mipya ya mwaka ujao. Bila shaka mipango hii inategemea sana rasilimali fedha, wapi utaipata na vipi utaitumia kwa ufanisi. Ni fursa itakayokufungulia milango ya kuumaliza na kuanza mwaka ukiwa na taarifa na maarifa juu ya rasilimali fedha. Itakupa fursa ya kujibu dukuduku lako juu ya nini ufanye na kwa kwa nini katika mazingira yako. Hii ni wiki inayolenga kushusha uchumi kwa mtu mmoja-mmoja kupitia maarifa.
Nchi nyingi duniani zinafanya kila jitihada kuwafanya raia wake kuwa na elimu juu ya masuala ya fedha kwa sababu hii ndiyo njia kuu ya kufanya uchumi uwafikie watu wengi. Marekani imetenga kila mwezi wa nne(April) kuwa mwezi wa uelewa wa masuala ya fedha kila mwaka, Uingereza , Brazil na India wana maadhimisho kama haya. Kwa hiyi uamuzi huu serikali ni mujarabu kwenye dunia ya leo. Ni uamuzi ambao unaakisi hoja ya kujenga uchumi wa watu.
Akitoa mada kwa Wahariri wa vyombo vya Habari juu ya Wiki ya Huduma za Fedha iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 1, Novemba, 2021; Bwana, Salimu Kamaro alisisitiza kuwa sekta ya fedha bado haijawafikia wananchi wengi kwa sababu ya uelewa na hivyo kuwafanya wabaki kwenye umaskini katikati ya itajiri mkubwa. Alieleza kuwa wiki hii itakuwa mwanga mpya katika jitihada nyingi za kufanya sekta ya fedha kuwa na majibu ya umaskini wa Watanzani.
Kwa kuwa na Wiki ya Huduma za Fedha ambapo wataalamu na watu wenye uzoefu kwenye sekta hii watatoa elimu kwa manufaa ya wengi; ni jitihada za kuhakisha uchumi unaokua unawafikia wananchi. Bi. Dionisia Mjema(Kmashna Msaidizi Wizara ya Fedha) anasema kuwa njia nzuri ya kuhakikisha sekta ya fedha inawanufaisha watu wengi nchini ni kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha wa masuala ya fedha na kuonesha kuwa Wizara itafanya maadhimisho haya kuwa ya kimkakati kwa lengo hilo.
Kama ambavyo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na maono ya kuwa; *Maendeleo ni yale yanayogusa watu*, Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inamulika ndoto hiyo ya baba wa taifa. Ni kupitia elimu hii watu wengi watakuwa kwenye uchumi jumuishi.
Ni muhali kwenye kasi ya sasa ya mabadiliko ya kiuchumi, kuwa na maendeleo ya wengi ikiwa wengi wako nje ya huduma za sekta ya fedha. Jitihada za Wiki ya Huduma za Fedha ni hatua nyingi mbele kwenye jitihada nyingi zetu kama nchi kujiletea maendeleo yetu wenyewe. Mwanya wa walio nacho na wasio nacho unaweza kupunguzwa kwa watu wengi kuwa na elimu ya masuala ya fedha.
Je unao uchaguzi nje ya kushiriki Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa? Jibu la swali hili lipo kwenye kauli mbiu ya maadhimisho haya ambayo ni *Boresha Maisha kupitia Elimu ya Fedha*
Chukua hatua, nafasi ni yako!!!