MBUNGE wa Jimbo la Welezo Mhe. Maulid Saleh Ali, akizungumza na Vijana mbalimbali mara baada ya kukagua matengenezo ya uwanja wa mpira wa miguu wa Matemwe katika Shehia ya Munduli.
************************
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MBUNGE wa Jimbo la Welezo Zanzibar Mhe. Maulid saleh Ali, amesema amejipanga kumaliza changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo ya jimbo hilo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akishirikiana na wananchi na mafundi wa Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) kusambaza mabomba ya maji katika shehia za Mtopepo na Munduli ndani ya jimbo hilo.
Alisema ni nishati muhimu kwa mahitaji ya kila siku ya wananchi kwani yanatumiwa katika matumizi mbalimbali ya msingi hivyo ni lazima yapatikane muda wote bila usumbufu.
Alisema ataendelea kushirikiana na Serikali kupitia mfuko wa jimbo kuhakikisha mahitaji yote ya msingi hasa maji safi na salama,elimu,huduma za afya,barabara za ndani na vikundi vya ujasiriamali kwa ajili ya kuwakwamua vijana na wanawake yote yanapatikana kwa wakati.
Katika maelezo yake mbunge huyo amewasisitiza wananchi hao kuwa walinzi wa miundombinu hiyo ya maji ili isihujumiwe na iweze kuendelea kuwanufaisha wananchi wengi na maeneo jirani.
“ Jimbo letu lina sifa kubwa ya kuwa na vyanzo vingi vya maji ambayo siku za hivi karibuni wamekuwa wakinufaika wananchi wa maeneo mengine huku baadhi ya maeneo ya jimbo letu yakikosa maji kutokana na changamoto za uchakavu wa miundombinu na uharibifu wa miundombinu hiyo na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.
Hivyo ni jukumu letu sote kama wananchi kuhakikisha tunaondosha changamoto hizo kwa kulinda miundombinu hii mipya huku tukilipia kwa wakati huduma za uendeshaji kwa mamlaka ya maji Zanzibar.’’, alisema Maulid.
Naye Diwani wa Wadi ya Munduli Juma Fikirini Khamis amewasihi wananchi wa maeneo hayo yanayokabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji pindi mradi huo mkubwa wa maji utakapokamilika wahakikishe wanajisajili na kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali.
Alisema viongozi wa jimbo hilo hasa Mbunge, mwakilishi wanashiri na madiwani wengine wanashirikiana vizuri kutatua changamoto za jimbo hilo kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Alieleza kwamba mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 900 wa shehia mbili na maeneo mengine.
Akizungumza fundi kutoka Mamlaka ya Maji Zanzibar(ZAWA)Talib Abdallah Mohamed, alisema wanatarajia kutumia mwezi mmoja kukamilisha zoezi hilo na kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya maji safi na salama.