***********************
Na Mwamvua Mwinyi,KIBAHA
SERIKALI imekopesha watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi bilioni 12.9 hadi kufikia Agosti mwaka huu fedha zitokanazo na asilimia 10 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kote nchini.
Aidha wenye walemavu hususani Wasioona wameaswa kuhakikisha wanajitokeza kushiriki zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 2022, ili kupata kujua idadi Yao kamili.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Naibu Waziri ofisi ya waziri mkuu sera, bunge na watu wenye ulemavu Ummy Ndeliananga wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe Kitaifa ambapo fedha hizo zimeweza kuwanufaisha watu wenye ulemavu.
Ndeliananga alieleza,watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa kama walivyo watu wanaoona na wanauwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi.
Alisema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuratibu na kuweka sawa mipango ya kisheria,kanuni na taratibu za watu wenye ulemavu katika kutetea haki zao na kutoa huduma za msingi.
Alisema kuwa, kutokana na hali hiyo ni lazima walemavu wote kupitia vyama vyao wakawa mstari wa mbele kujitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya mwaka 2022 ili kuisaidia Serikali katika kuwafikia Walemavu wote waliopo nchini.
“Ndugu zangu tunapoadhimisha Leo siku ya Fimbo Nyeupe ni lazima pia tukumbuke suala la Sensa lililopo mbele yetu na mimi Waziri wenu nachukua fursa hii kuwaomba wenzangu twende tukahamasishane kushiriki Sensa hiyo kwa faida yetu na faida ya Taifa letu,”alisema Waziri Ndeliananga
Mbali na Sensa lakini pia Ndeliananga amewakumbusha watu wote wenye ulemavu nchini kuhakikisha wanajitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe na familia zao.
Naye Margareth Matonya mkurugenzi anayeshughulikia watu wenye mahitaji maalumu kutoka wizara hiyo alisema kuwa mwaka huu wametoa mafunzo kwa walimu na 1,373 wathibiti ubora 200 kwa lengo la kukagua miundombinu kama inafikika eneo la ujifunzaji na ufundishaji na wanaangalia walimu wanavyofundisha wanafunzi wenye ulemavu.
Awali mwenyekiti wa Cham Cha Wasioona TLB Omary Sultan alisema kuwa maadhimisho hayo ni kwa ajili ya kukaa na kutafakari masuala mbalimbali ya wanachama ili kujua changamoto na mafanikio na kujifunza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, kijamii, afya na masuala ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kibaha Sara Msafiri ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema kuwa mkoa huo umejenga mabweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwenye Halmashauri Chalinze na Mkuranga.
Alisema kuwa anaendelea kushirikiana na Walemavu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo hususani katika kuweka misingi yao imara.