****************************
Na Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaa, inaendelea na hatua ya uboreshaji wa zone ya kukaangia samaki katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri.
Pamoja na ukarabati mkubwa uliofanyika, pia imeanza kufunga majiko mapya ya kisasa ya kukaangia samaki yanayo tumia gesi kidogo.
Diwani wa Kata hiyo Sharik Chougle,ameyasema hayo leo wakati alipoongoza kamati ya soko kitengo cha Ugavi kukaagua majiko mapya 24 kati ya 48 ambayo Halmashauri hiyo inatarajia kuyafunga katika soko hilo yanayozalishwa na kampuni ya Envotec, iliyopo Mtaa wa Luichi Kinondoni,.
“Awali Halmashauri ya Jiji ilichukua majiko 24 kutoka Envotec na yamebaki majiko 24, ambayo ndiyo tumefika kuyakaagua,”alieza Choghle.
Diwani huyo akiwa na Afisa Ugavi na Manunuzi wa Halmashauri hiyo ya Jiji katika Soko la Feri Agatha Mbunda, alisema dhamira ni kuwaboreshea huduma wakaangaji samaki na wateja katika soko hilo bora katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.
Mkurugenzi wa Envotec Services Limited , Sauli Mwambije, alishukuru Halmashauri ya Jiji kwa kuthamini mchango wa kazi za wazawa na kueleza kuwa majiko hayo ni bora, rafiki wa mazingira na hulinda thamani ya fedha.