Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Uwekezaji,Geoffrey Mwambe,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 3,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Uwekezaji,Geoffrey Mwambe,akielezea zaidi mafanikio ya wizara yake wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru leo November 3,2021 jijini Dodoma.
Waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Uwekezaji,Geoffrey Mwambe wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru leo November 3,2021 jijini Dodoma
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIKA jitihada za kuhamasisha uwekezaji wa kimkakati nchini Serikali imefanikiwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali, ujenzi wa miundombinu utoaji wa elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji.
Hayo yameelezwa leo Novemba 3,2021 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Uwekezaji,Geoffrey Mwambe wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.
Waziri Mwambe amesema kutoka Tanzania ipate uhuru, Serikali imechukua hatua ya makusudi ya kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa wananchi katika uchumi.
Amesema Serikali imepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali, ujenzi wa miundombinu utaoaji wa elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine za kuandaa, kusimamia na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo sheria, kanuni na maelekezo yote yanayohusu uwekezaji ili kuhakikisha kuwa vikwazo vyote katika uwekezaji vinatambulika na kuondolewa pamoja na kuwa na mazingira rafiki na sawa katika uwekezaji.
Aidha amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ambayo yatasaidia wananchi na sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarisha miundombinu ili kupunguza gharama za uzalishaji.
“Kutengwa kwa maeneo ya biashara, kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na miradi mikubwa ya uwekezaji, kuboresha utoaji wa mikopo kwa kupunguza riba na masharti mengine, kutoa elimu kwa wajasiriamali na kudhamini mikopo kwa wajasiriamali,”amesema.
“Vipo Viwanda vipya vilivyowahi kujengwa ambavyo havikuzalisha kabisa, au vilichelewa sana kuanza kuzalisha na hatimaye pia vikazalisha chini ya kiwango cha uwezo kilichowekezwa.
“Uamuzi wa kusambaza Viwanda nchini ili kusawazisha maendeleo ulisababisha mara nyingine Viwanda kujengwa mahali ambapo hakuna maji, au umeme, au vyote viwili, bila kusahau hali duni ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji,”amesema
Amesema kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, uwekezaji wa ndani na ule wa kutoka nje umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mafanikio hayo yanaweza kupimwa kwa vigezo vitatu vinavyotumika kupima kiwango cha uwekezaji kwa nchi ambavyo ni Uwiano wa Uwekezaji na Pato la Taifa, pamoja na Kiwango cha Uwekezaji Kutoka Nje na kiwango cha Ukuzaji Rasilimali kwa kila mwaka.
Amesema tangu Serikali ilipoanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, wastani wa uwekezaji unaopimwa kwa kuangalia uwiano wa uwekezaji yaani Ukuzaji Rasilimali kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka.
“Takwimu zinaonesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa umekua kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019. Hivi ni viwango vikubwa ukilinganisha na wastani wa nchi za Afrika wa asilimia 21 – 22 na nchi zilizoendelea wa asilimia 23 hadi 25,”amesema.
Waziri Mwambe amesema uwekezaji wa mitaji kutoka nje umekuwa ukiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 0.73 mwaka 1996 hadi Dola za Marekani bilioni 2.18 mwaka 2013 na hadi Dola za Marekani bilioni 1.01 mwaka 2020.
“Serikali imefanikiwa kuanzisha Kituo cha Utoaji Huduma za Uwekezaji Mahali Pamoja kwa kuleta pamoja Wizara na Taasisi 12 ambazo ni Wizara ya Kazi (masuala ya vibali vya kazi), Wizara ya Ardhi (masuala ya Ardhi-Derivative rights), Idara ya Uhamiaji (Masuala ya vibali vya ukaazi, TIC (kuratibu na kutoa Cheti cha Vivutio), BRELA (Usajiri wa Kampuni), NIDA, TBS, NEMC, OSHA, TRA, TMDA na TANESCO,”amesema.
Waziri Mwambe ameyataja mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa Usajili wa miradi ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 (sawa na shilingi trilioni 8.050 ambapo amedai miradi hiyo itatoa ajira za moja kwa moja el 38,000.
“Taarifa ya ulinganifu kwa kuzingatia miradi iliyoandikishwa TIC peke yake katika kipindi cha miezi sita ni 164 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.158 sawa na Shilingi za Tanzania trilioni 7.267.
“Usajili wa miradi hii ni sawa na ongezeko la takriban asilimia 500 ikilinganishwa na usajili kwa kipindi kama hiki mwaka jana ambapo miradi iliyosajiliwa ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 647.43,”amesema
Ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya ajira zinazotarajiwa kutokana na Miradi iliyoandikishwa ambapo ajira 38,000 zitapatikana kwa ujumla.
Pia,kupungua muda wa upatikanaji vibali vya kazi ambapo katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuondoa urasimu wa upatikanaji vibali vya kazi hivi sasa hata ndani ya siku moja mwombaji anaweza kupatiwa kibali kupitia mfumo wa ki elektriniki (e-permit).
Amesema Mfumo huo unaruhusu pia upatikanaji wa kibali cha ukaazi katika kadi moja ambapo kabla ya hapo kibali kilichukua hadi miezi sita na maombi mengi yalikuwa yanakataliwa baada ya mwombaji kulipa.
Pia,Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya kuratibu ajira za wageni ambapo kwa sasa sheria inaruhusu sheria inaruhusu mwekezaji kuingiza wataalamu 10 kutoka watano ilivyokuwa kabla ya Oktoba 2021.
“Uanzishaji Kituo cha Mawasiliano kwa Uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Call Centre) kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha uundwaji wa mfumo wa ufuatiliaji malalamiko ya wawekezaji na kuwapatia taarifa sahihi kituo hiki kimeanzishwa na kinafanya kazi kwa ufanisi;”amesema.
Pia,Wizara iliratibu ubainishaji wa changamoto za uwekezaji kwa kuwataka wawekezaji kuwasilisha changamoto zao ambapo Ofisi ilipokea changamoto 112 kutoka katika kampuni 92.
Vilevile,Serikali imewezesha upatikanaji wa Uwekezaji wa Miradi yenye manufaa makubwa kiuchumi ikiwemo ya Kampuni ya Elsewedy wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tatu ($3bn.
Amesema Serikali imendelea kuimarisha majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kutafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta binafsi ili kukuza uchumi na kuiwezesha sekta binafsi kuwa injini ya uchumi.
Waziri Mwambe amesema hadi Juni, 2021 kuna Vyama vya Ushirika 9,185 vyenye jumla ya wanachama 6,050,324 ambapo wanaume 3,932,711 na wanawake 2,117,613.
Amesema kati ya vyama, Vyama vya Ushirika wa Masoko ya Mazao (AMCOS) vilikuwa 4,039 vyenye jumla ya wanachama 2,660,562, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vilikuwa 3,831 vyenye jumla ya wanachama 2,523,548.
Amesema Vyama vya Msingi vilikuwa 58 vyenye jumla ya wanachama 38,206, Vyama vya Joint enterprises vilikuwa 42 vyenye jumla ya wanachama 27,666 na Vyama vingine (katika sekta mbalimbali) vilikuwa 1,215 vyenye jumla ya wanachama 800,342;
“Kuanzisha Vituo vya Uwezeshaji 17 katika Mikoa ya Singida (1), Shinyanga (1) Kigoma (6), Dodoma (7), Rukwa (1) na Geita (1) kama iliyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 katika Ibara ya 26,”amesema.