Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Sara Msafiri akiongozana na baadhi ya viongozi wengine kwa ajili ya kukagua ujenzi wa mradi wa daraja hilo la Lumumba lililopo kata ya Pangani.
*************************
NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Mhe.Sara Msafiri ameendelea na utaratibu wake wa kufanya ziara kwenye kata ambapo ametembelea kata ya Pangani na Mkuza kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili Wananchi.
Mkuu huyo katika ziara yake ambayo aliambatana na viongozi mbali mbali wa serikali alitembelea na kujionea mradi wa ujenzi wa Daraja la Lumumba ambalo linaunganisha Wilaya Mbili za Kibaha pamoja na Ubungo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kutokana na kupata shida ya kuvuka wakati wa mvua.
Alisema kuwa ana Imani kubwa ujenzi wa daraja hilo pindi utakapokamilika itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo ya Pangani pamoja na maeneo mengine ya jirani kuweza kupita kwa urahisi.
Akizungumzia Daraja hilo,Diwani wa kata ya Pangani Mheshimiwa Augustino Mdachi alibainisha kuwa wananchi wake wamekuwa wakisumbuka Sana kuvuka katika eneo hilo.
Aidha alifafafanua kuwa kwa kipindi Cha muda mrefu wananchi wanapata kero kubwa hivyo mwaka 2016 aliwaandika jeshi la wananchi Tanzania kuwaomba daraja la muda na kupewa lililokuwa Mpwapwa lenye uwezo wa kupitisha uzito usiozidi tani 10 .
Mdachi alifafanua kuwa daraja hilo la muda kilikuwa linasafirishwa kwa msaada wa kampuni ya Madalali wa Bima Tanzania kwa kuchangiwa mafuta ya shilingi 15 milioni.Aidha, Msaada wa kulifunga ulifanywa na benki lenyewe kwa ushirikiano wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA.
Naye Kaimu Meneja wa TARURA Kibaha Donald Mjale amesema kuwa katika kukamilisha Daraja hilo serikali kupitia TARURA Imeshatumia milioni 80 kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa kokoto tani 60,waya,bolt nakuchimba mtaro wa kuchepusha njia za maji ili kupunguza hatari ya kuharibu kingo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amewataka TARURA kuweka jicho la kitalam na ubunifu kwenye Daraja hilo kuwa bado utaalam wao unahitajika ili kuliweka kwenye kiwango bora.
Aidha Mhandisi Munde amewashauri kuweka alama za barabarani ili kutoa tahadhari na kujiridhisha na uzito unaotakiwa kwani kutokana na umri wa vyuma vya daraja hilo kuwa chakavu inashauriwa isizidi tani 5.
Munde amemuomba Diwani wa kata kufanya ufuatiliaji jeshini kupata taarifa zaidi ya daraja hilo kama limetolewa jumla au limeadhimishwa na iwapo watakuwa wametoa kwa muda basi mamlaka inayohusika iweke mikakati ya kujenga daraja la kudumu siku zijazo.
Akihitimisha ziara hiyo Mkuu wa Wilaya,Sara Msafiri amewashukuru wananchi kwa kujitoa kuchangia ujenzi wa daraja hilo ambalo kukamilika kwake litawaondolea adha kubwa waliyokuwa wakiipata wananchi.