MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Ndugu Leila Burhan Ngozi akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya pongezi za CCM kwa utendaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi katika utendaji kwa kipindi cha mwaka mmoja.
*****************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar kimesema kwamba kimeridhishwa na utendaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, ambaye kwa kipindi cha mwaka mmoja toka aapishwe amedhibiti vitendo vya rushwa,ubadhilifu wa mali za umma na kuwaunganisha Wananchi kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kauli hiyo ameitoa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Ndugu Leilah Burhani Ngozi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari huko Afisi Kuu ya ccm Kisiwandui Unguja juu ya utendaji wa Rais huyo kwa kipindi cha mwaka mmoja toka aingie madarakani.
Alisema ndani ya Kipindi cha mwaka mmoja Rais Dk.Hussein, ametekeleza mambo mengi ya maendeleo ikiwemo kudhibiti mianya ya rushwa na upotevu wa fedha katika taasisi mbalimbali za umma hasa katika maeneo ya Bandari na Viwanja vya Ndege Zanzibar hali iliyosababisha kuongezeka kwa mapato na kupaa kwa uchumi wa Zanzibar.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu Ndugu Ngozi, alisema pia Rais huyo ameendeleza mapambano dhidi ya Dawa za kulevya sambamba na kuthibiti vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambapo hivi karibuni amemteua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Naibu wake ambao kwa mara ya kwanza nafasi hizo kuteuliwa mwanamke ili aweze kushughulikia kesi hizo na kuzimaliza kabisa.
Alisema katika juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi Rais Mwinyi, amefungua milango ya uwekezaji kwa kuzungumza na Wawekezaji mbalimbali wa Kimaifa kuja nchini kujenga Mahoteli na Viwanda ili wananchi wapate ajira kwa lengo la kutekeleza maelekezo ya Ilani ya CCM ya kufikia ajira 300,000 kwa Vijana wa Zanzibar.
Pamoja na hayo amesema kwamba Rais Mwinyi katika utawala wake alielekeza Wananchi wa Pemba kupewa umiliki rasmi wa mashamba ya mikarafuu ambayo awali yalikuwa yakikodishwa kwa wananchi hao chini ya usimamizi wa Serikali.
Ngozi, alieleza kwamba Dk.Mwinyi, amekuwa akihimiza suala la usafi wa Miji na Jiji pamoja na mazingira kwa ujumla kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inakuwa safi kutokana na uchumi wake kutegemea Sekta ya Utalii.
“Chama cha Mapinduzi tunampongeza Rais wetu Dk.Hussein Ali Mwinyi amefanya mengi kwa kipindi kifupi na bado ana mipango mbalimbali ya kutuletea maendeleo, hivyo tunawaomba wananchi waendelee kumuunga Mkono kwa kulipa kodi na kufanya kazi kwa bidii.
Pia kwa sasa tunashuhudia namna Rais wetu anavyoweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali mikubwa yakiwemo Mahoteli ya Kimataifa ambayo ni fursa kubwa ya ajira kwa wananchi wetu kupitia sekta ya Utalii huku akisisitiza vijana wa eneo husika ndiyo wapewe kipaumbele cha ajira hizo . ”, alisema Ngozi.
Katika maelezo yake Mjumbe wa Kamati Kuu huyo Ngozi, alisema Serikali imekuwa ikiwajali wananchi hasa katika suala la Mafuta ya Petrol kupanda katika soko la Dunia lakini Rais alitoa tamko la serikali kubeba mzigo huo na kuhakikisha wananchi wanapata Nishati hiyo kwa bei rafiki zinazoendana na kipato cha wananchi.
Pamoja na hayo alisema hivi karibuni Wananchi wanaoishi katika Nyumba za Maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini zinazosimamiwa na Shirika la Nyumba Zanzibar, kulalamika kwa malimbikizo ya madeni Serikali ilielekeza wasifukuzwe na badala yake wawekewe utaratibu wa kulipa kidogo kidogo ili zipatikane fedha za kujengwa kwa Nyumba mpya.
Aidha Mjumbe huyo alisema Serikali imeahidi kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara za ndani zitakazokuwa na urefu wa kilomita 275 kwa Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo ameeleza kwamba Rais wa Zanzibar Dk.Hussin amekuwa karibu na viongozi wa dini mbalimbali ambao wamekuwa wakisaidia kuhimiza umuhimu wa Amani na Mshikamano kwa wananchi.
Alisema kwamba Serikali ya awamu ya Nane imeendelea kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19.
“Tunawasihi wananchi waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ya ugonjwa huo na kuendelea kujitokeza kwa wingi kuchanja kwa hiari kwani bado ugonjwa huo ni tishio Duniani, licha ya Wizara yetu ya Afya Zanzibar kutangaza kuwa Wagonjwa wa maradhi hayo wamepungua ni muhimu tuendelee kujikinga na kufuata maelezo ya wataalamu.”, alifafanua Ngozi.
Alisema CCM Zanzibar inampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi yake ya kushirikiana vizuri na Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi, kwa maamuzi yake ya kuipa Zanzibar fungu la fedha zilizotolewa na Shirika la fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya maendeleo ya mradi ya UVIKO-19 kwa upande wa Tanzania.
Pamoja na hayo amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu imepokea msaada wa dola za kimarekani milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwa lengo la kuondoa uhaba wa madarasa katika skuli zenye wanafunzi wengi madarasani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi hao kufeli.
Alifafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni amesema kuwa mazungumzo yapo katika hatua nzuri ya kuipatia Zanzibar mkopo nafuu wa ujenzi wa mradi mkubwa ya Hospitali ya rufaa ya Binguni.
Pamoja hayo alisema kwamba Chama Cha Mapinduzi kinaridhishwa na ushirikiano mkubwa wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 unaofanywa na Serikali zote mbili ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema kwamba CCM inaendelea kuwataka Viongozi na Watendaji wa Serikali kuendelea kuwa waaminifu na kuepuka vitendo vya wizi wa mali za umma na badala yake wafanye kazi kwa bidii ili Nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia malengo ya Rais Mwinyi ya Zanzibar kukua kiuchumi kupitia Falsafa ya Uchumi wa Blue.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anatimiza mwaka mmoja toka aingie madarakani aliapishwa mnamo Novemba 3, mwaka 2020 ambapo leo (3) kesho anatimiza mwaka mmoja toka aingie mararakani.