……………………………………………………………..
Na Damian Kunambi, Njombe.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere amewataka madiwani pamoja na watendaji wa kata zote za wilaya hiyo kusimamia vyema fedha za miradi za UVIKO – 19 bilioni 1.8 ambapo milioni 920 kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 47 na zaidi ya milioni 978 miradi ya maji.
Akizungumzia mradi wa vyumba vya madarasa amesema wilaya hiyo ina shule za sekondari 17 hivyo kila shule inatakiwa kujengewa vyumba vya madarasa visivyopungua viwili kwa gharama ya shilingi milioni 20 kwa kila chumba.
Ameongeza kuwa anaweka ushindani kwa kila eneo litakalojenga vyumba hivyo kwa wakati ambapo ujenzi huo unatakiwa kumalizika December 15 hivyo watapangwa washindi kulingana na muda waliotumia kumaliza ujenzi na watatangazwa hadharani.
“Leo kwa pamoja tunakubaliana hapa kuwa tunaweka ushindani, itakapofika muda wa kutangaza washindi na wewe ulioshindwa tutakutangaza sasa usije ukasema mkuu wa wilaya ananidhalilisha wakati wewe ndo umejidhalilisha maana hii kazi tunaanza pamoja kwanini wewe ubaki nyuma? “, Amese Tsere.
Aidha kwa upande wa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias amesema kuwa fedha hizo tayari zimeshafika wilayani na utekelezaji wake tayari umeanza ambapo baadhi ya kata tayari wameanza hatua za awali za kukusanya mawe pamoja na mchanga.
Pia ameunga mkono suala la kushindanisha shule zitakazomaliza ujenzi kwa mapema na kuongeza kuwa wataangalia uwezekano wa kuandaa vyeti kwaajili ya kuwakabidhi washindi hao kuanzia wa kwanza hadi wa tatu.
” Lengo letu ni kushika nafasi ya kwanza kwa mkoa wa Njombe kwani tayari tulishapewa maagizo kutoka kwa mkuu wa mkoa hivyo kwakuwa wanaludewa ni wapenda maendeleo natumai suala hili tutalisimamia vyema”, amesema Deogratias.
Wise Mgina ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo amesema fedha za mradi wa maji zimegawanywa katika kata mbili ambapo kata ya Ludewa mjini imepata kiasi cha shilingi milioni 450 ambazo zitatumika kurekebisha mifumo ya maji na zaidi ya milioni 528 zimeelekezwa katika kata ya Madope kwaajili ya kukamilisha mradi wa maji.
Amesema kuwa fedha hizo zimegawiwa maeneo mawili ili kupunguza changamoto za maji kwa awamu kwani wakisema wagawe kila mahali kidogo kidogo hawawezi kumaliza tatizo hivyo ni bora kuweka nguvu sehemu moja na kumaliza tatizo sehemu moja kwenda nyingine.