Wawezeshaji wa Uundaji wa Vikundi vya Huduma Ndogo za Kifedha kwa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) wameanza kupatiwa mafunzo ya siku tano Wilayani Busega, mafunzo yaliyoanza tarehe 02 Novemba 2021.
************************
Nae mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Juma Rahisi amesema kwamba ni nafasi kubwa wamepewa washiriki na wameaminiwa kushiriki katika zoezi hilo, hivyo hawana budi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa. “Mmeaminiwa kufanya kazi iliyopo mbele yenu kwani wengi wangeweza kuchaguliwa kushiriki katika zoezi hili, lakini kwa nafasi ya pekee mmepata nafasi, hivyo mnatakiwa kutumia vizuri nafasi hiyo, aliongeza Bw. Juma Rahisi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF Kitaifa Bi. Nuru Mkomambo amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hilo ni vyema washiriki kuwa makini wakati wa mafunzo hayo yatakayofanyika kwa siku tano kabla ya kuelekea kwa walengwa kwaajili ya uundaji wa Vikundi vya Huduma Ndogo za Kifedha.
Bi. Mkomambo amesema katika kipindi hiki cha Awamu ya tatu kipindi cha pili TASAF inalenga katika kuwezesha Kaya kufanya kazi ili kujiongezea kipato kupitia utekelezaji wa ajira za muda kwa walengwa pamoja na kuhamasisha uwekaji wa akiba na kutekeleza shughuli za kukuza uchumi wa Kaya.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Wilaya ya Busega Bi. Wema Mmari amesema zoezi la mafunzo linatarjiwa kufanyika kwa siku tano na baadae Washiriki wa mafunzo hayo watafanya zoezi la kuhamasisha Walengwa wa TASAF kwaajili ya kuunda Vikundi vya Huduma Ndogo za Kifedha. TASAF III kipindi cha pili inatekeleza zoezi la uundaji wa vikundi huku vijiji 41 vilivypo kwenye Mpango wa TASAF Wilayani Busega vinahusishwa kwenye mpango huo ambapo matarajio ni kuundwa vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha zaidi ya 200.