Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MKURUGENZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Paradise Mission Ndele Mwaselela iliyoko mkoani Mbeya amewaonya Vijana nchini kutozingatia kauli za Wanasiasa ambazo zinaweza kuwakatisha tamaa katika kutafuta maendeleo yao na badala yake wafanye kazi kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao.
Mwaselela ametoa wito huo jijini Mbeya wakati akizungumza na kundi la waandishi wa habari Wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini, wanaofanya ziara ya kutembelea vivutio vya Utalii nchini ambapo awamu hii wanaangazia mkoa wa Mbeya.
Amesema kuwa ili vijana kufikia malengo yao wanapaswa kufanya kazi kwa bidii bila kuhofia maneno ya wanasiasa kuwa kufanikiwa kwao Kuna lengo la kutaka kugombea nafasi mbalimbali kisiasa.
“Ukifanikiwa lazima usaidie Jamii katika mambo mbalimbali sasa kwa Upande wana siasa hasa wa Mkoa wa Mbeya wakiona kijana aliyefanikiwa anasaida Jamii unaambiwa unalengo la kugombea kwenye majimbo yao jambo hili linaweza kurudisha nyuma jitihada za vijana hawa katika kusaidia jamii”amesema Mwaselela.
Pia amewataka vijana kutorudi nyuma wanapoamua kujiinua katika kiuchumi hasa katika kusaidia jamii inayowazunguka kwakuwa uwekezaji unahitaji kusimamia misimamo na nia zao katika kufikia mafaniko waliyojipangia.
“Wanasiasa hao kuacha kuogopa maendeleo ya vijana na badala yake wawape ushirikiano katika kuinua miradi yao kwakuwa wote Jamii inawahitaji katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo,…..
“Wanachoongea jukwaani kuhamasisha vijana kujituma ni tofauti na matendo yao wao wanachowaza ni kuporwa majimbo yao waache Jambo ambalo halina tija kwa Vijana, Serikali ina nia nzuri na vijana katika kuwainua kimaendeleo,”amesema Mwaselela.