******************************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Wakinamama wajawazito wanaosubiria kujifungua ambao wanaishi katika majengo ya hospitali ya wilaya ya Ludewa yajulikanayo kama kambi ya wajawazito wameulalamikia uongozi wa hospitali hiyo kuwalipisha gharama ya malazi hivyo wameuomba uongozi huo kuwapunguzia ama kuwaondolea malipo hayo.
Wakitoa malalamiko hayo wakinamama hao wamedai kuwa wamekuwa wakilipishwa kiasi cha shilingi elfu 8 ambapo shilingi elfu 5 ni gharama ya mama mjamzito na shilingi elfu tatu kwaajili ya muuguzi wake kitu ambacho kinawaongezea gharama za huduma hospitalini hapo.
Monica Haule ni mmoja wa akina mama hao amedai kuwa awali malipo hayo hayakuwepo hivyo anashangazwa safari hii amefika kambini hapo na kupewa taarifa kuwa hatakiwi kulala hapo bila kufanya malipo hayo.
” Huu utaratibu ni mpya kwangu kwani kipindi cha nyuma hakukuwa na haya malipo na nilipoambiwa nilipe hiyo hela sikuwa na namna zaidi ya kulipia japo inatuongezea gharama kwani tunatoka mbali na tunamahitaji mengi kwaajili ya maandalizi ya kujifungua hivyo tunaomba serikali ituhurumie”, Amesema Bi. Haule.
Naye Witness Mwinuka amedai kuwa nje ya malipo hayo ya malazi wamekuwa wanapowasili hospitalini hapo bila barua ya daktari walikotoka huambiwa walipie kiasi cha shilingi elfu tano na endapo wasipofanya hivyo hawatapata huduma.
Aidha kwa upande wa wauguzi wa wajawazito hao wamedai kuwa mazingira wanayolala si rafiki kwao kwani jengo wanalotumia halina milango wala madirisha na wanaweka magodoro chini kitu ambacho kinaweza kuathiri afya zao.
Sanjali na hilo pia wamesema jiko wanalotumia ni dogo hivyo wanalazimika kupikia nje hivyo wanaiomba serikali kuwatatulia changamoto hizo.
Katika hatua nyingine suala hili linafika katika kikao cha baraza la madiwani na kujadiliwa ambapo madiwani hao wamehoji juu ya mchakato uliotumika katika kupitisha gharama hizo wanazolipishwa wakina mama hao na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutoa maelezo juu ya malipo hayo.
Akiwasilisha hoja hiyo diwani wa viti maalum tarafa ya Mawengi Marry Mapunda ametaka gharama hizo zisitishwe kwani kinamama wanapokuwa katika hali ya ujauzito hupitia wakati mgumu na huwa na matumizi makubwa huku baadhi ya madiwani wakiungana naye katika hoja hiyo.
Hata hivyo kwa upande wa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias amesema kiwango kinacholipishwa ni shilingi elfu tano ambapo shilingi elfu mbili kwaajili ya muuguzi na shilingi elfu tatu kwaajili ya mama mjamzito.
Amesema fedha hizo hulipishwa kwaajili ya kuendeshea huduma za jengo hilo ikiwemo umeme, maji pamoja na kukarabati majengo hayo.
“Naomba waheshimiwa madiwani mniunge mkono katika hili ili tuweze kuendesha huduma za pale pamoja na kuboresha majengo, kwa makusanyo hayahaya madogo tayari tumeweza kukarabati jengo la wajawazito na tunatarajia kufanya hivyo pia katika jengo la wauguzi pamoja na jiko”, Amesema Deogratias.
Suala hili bado halijafikiwa muafaka ambapo mmoja wa wajumbe wa baraza hilo ambaye ni diwani wa kata ya Ibumi Edward Haule aliliomba baraza kulikabidhi jambo hilo katika kamati husika ili liweze kujadiliwa kwa undani.