Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Suzana Raymond akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani.
*******************************
NA VICTOR MASANGU,PWANI
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Suzana Raymond amewaonya wanaojihusisha na Rushwa kwenye miradi ya maendeleo kuacha mara moja kwani Taasisi hiyo haitawavumilia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Suzana ametoa onyo hilo jana alipokuwa akizingumza na waandishi wa habari ambapo alitoa taarifa ya miezi mitatu ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo.
Alisema TAKUKURU itakuwa macho muda wote kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezeka kwa kiwango kinachotakiwa kwani ndio njia sahihi ya kumsaidia mwananchi kupata huduma za kijamii.
” Tutahakikisha ukaguzi wa miradi unafanyika kila wakati kuwabaini wote wwnyw lengo ovu, niwaombe wana Pwani msisite kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwenye miradi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kwa wakati” alisema.
Alisema TAKUKURU itaendelea kufuatilia fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa lengo la kudhibiti ubadhilifu na pale itakapobainika wahusika watachukuliwa hatua.
Alieleza kuwa Taasisi hiyo itaendelea kuelimisha Umma kuhusiana na madhara ya Rushwa ili waifahamu nafasi yao katkka mapambano ya Rushwa kwani vita hiyo ni ya Watanzania wote.
Suzana pia alisema utafanyika utafiti katika vyuo vilivyopo kwenye mkoa huo kuona visababishi vya Rushwa ya ngono.
Alisema wataendelea kuanzisha klabu za wapinga Rushwa shuleni ili elimu hiyo ianzie ngazi za chini na kuandaa kizazi kinachopambana na vitendo vya Rushwa.