Huu ni mfano wa namna wawekezaji wanavyopunguza gharama za matumizi ya umeme wa gridi ya Taifa kwa kutumia nishati jadidifu ya umeme unaozalishwa kwa jua(solar Power) kuchemsha maji.Picha hii nimepiga katika moja ya jengo la hoteli ya Oceanic Bay iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani ikiwa na maana kuwa matumizi ya nishati jadidifu yameendelea kupewa kipaumbele na wawekezaji (PICHA NA ALEX SONNA )
……………………………………………………
Na Selemani Msuya
NISHATI Jadidifu ni nishati inayozalisha umeme utokanayo na vyanzo asilia kama vile mwanga wa jua, upepo, kinyesi, maji, jotoardhi, makaa ya mawe, chuma kutoka ardhini na hudumu kwa muda mrefu.
Inatajwa kuwa ina faida za kijamii, kiuchumi na maendeleo kwa jamii na nchi kwa ujumla hasa kutokana na kutunza mazingira na gharama ndogo.Mikakati ya dunia nzima kwa sasa ni kuhakikisha nishati hiyo inapewa nafasi hiyo ikiwa ni kutokana na usalama na ubora wake ambao haudhuru viumbe hai.
Umoja wa Mataifa (UN), kupitia lengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs), lengo la saba linasisitiza ifikapo 2030, nishati iwe inapatikana kwa urahisi, uhakika, endelevu na ya kisasa.
Tanzania kupitia viongozi wake wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hapo nyuma katika kuhamasisha uzalishaji wa nishati jadidifu ili iweze kushirikiana na nishati inayotokana na vyanzo vya maji na mafuta anasema “Kutokana na kasi ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kuchanganya vyanzo vya nishati ili kuwa na uhakika wakati wote.
“Hivyo basi tunaangalia uwezekano wa kutekeleza miradi ya nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi), kwa kuwa vyanzo hivi ni endelevu, tunatarajia katika miaka hii mitano kuzalisha Megawati 1,100 kupitia vyanzo hivyo.”
Lengo hilo la Rais Samia linaungwa mkono na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mipango na mikakati ya Wizara ya Nishati na wadau mbalimbali.
Kifungu cha 63 kifungu kidogo (h) cha Ilani ya CCM, kinaelekeza kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme wa kutosha na wa gharama nafuu kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji, gesi asilia, makaa ya mawe na nishati jadidifu (jotoardhi, upepo, jua na tungamotaka).
Sera ya Nishati ya Taifa ya 2015 imeanishwa na lengo la 7 (Nishati Safi na Nafuu) kwenye msisitizo wa kupeleka umeme vijijini. Shabaha yake ni kuwezesha matumizi ya rasilimali za nishati jadidifu ili kuongeza mchango wake kwenye uzalishaji wa umeme wote.
Mpango wa Nishati Endelevu kwa Wote Ajenda ya Mustakabali wa Tanzania (SEforALL AA) unachukuliwa na Serikali kama nyenzo ya kutekeleza lengo la 7.
Moja ya mdau wa kwanza kuzalisha nishati jadidifu na kuweza kuuzia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusambaza kwa wananchi ni Kamapuni ya Nishati ya Rift Valley (RVE).
RVE ni kampuni inayopatikana katika kijiji cha Mwenga wilayani Mufindi mkoani Iringa ambapo pia wana kampuni nyingine ya kilimo biashara ya Rift Valley Holdings (RVH), ambayo ni moja ya kampuni kubwa ya kilimo biashara Afrika.
Meneja Mkuu wa RVE, Deo Massawe anasema wameanzisha Mradi wa Kuzalisha Umemem wa Mwenga ambao umeweza kung’arisha kijiji na kuchochea maendeleo kwa kasi.
Massawe anasema wamefika katika vijiji 34 hadi sasa ambavyo zaidi ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika vilikuwa havijapatiwa umeme pamoja na ukweli kuwa chanzo cha umeme Kihansi kipo karibu nao.
Anasema kuanzia mwakwa 2012 hadi 20202 wamefakiwa kuzalisha nishati katika maeneo matatu tofauti ambapo wamezalisha megawati 7.4 ambazo zinatokana na umeme maji na upepo.
Masawe anasema wamefanikiwa kusambaza umeme katika eneo lenye ukumbwa wa kilomita 460 na kunufaisha watu 70,000 wa kaya 5,500 za Mufindi na Njombe ambapo kazi ya usambazaji inaendelea.
Meneja huyo anasema mikakati yao RVE ni kusambaza nishati jadidifu kwenye kaya 12,000 ifikapo mwaka 2024, huku wakiendelea na maandalizi ya kuzalisha megawati 8.5 na kuendeleza chanzo kimoja wilayani Tukuyu na kunufaisha watu 50,000, vijiji, taasisi, SMEs na viwanda vya ndani vya chai.
“Sisi RVE kupitia mradi wa Mwenga ni wamiliki na waendeshaji mradi wa kibiashara na kupata leseni ya kusambaza na kuuza kwenye gridi ya taifa.
Anasema kupitia mradi wa Mwenga wamefanikiwa kuzalisha umeme wa maji megawati 4 na 2.4 wa upepo kwa kaya 5,500.
Massawe anasema umeme huo wa kisasa ambao wanazalisha umesambazwa kwenye viwanda vya chai viwili, maziwa kimoja, vya mbao viwili na vikundi vingine vingi ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali.
“Umeme wetu ni wa bei nzuri ambapo watumiaji wadogo D1 wanaotumia umeme usiochozidi 50 wanatozwa Sh 60 na wale wa T1 Sh 243.04,” anasema.
Massawe anataja baadhi ya vijiji vinavyonufaika ni pamoja na Usukani, Ukonge na vingine, ila pia wameanzisha vijiji vingine sita katika mkoa wa Njombe.
Anasema megawati 2.4 inasambazwa kwenye vijiji 34 vya Mwenga ambapo kupitia nishati hiyo vijiji vyote vimeweza kupata maendeleo.
Meneja huyo anasema uwekezaji wa kuzalisha nishati uliokamilika ni Mufindi na Njombe ambapo wanazalisha megawati 7.4 huku mipango yao ikiwa baada ya miaka mitatu kuongeza megawati 8.4 katika Wilaya ya Tukuyu.
“Katika mradi huo wa wilayani Tukuyu utagharimu zaidi ya Sh bilioni 20 na kuongeza wanufaika wa nishati hadi kufikia laki moja kwenye kaya 8,000 hadi 12,000 ifikapo 2025,” alisema.
Anasema uwepo wa nishati katika vijiji umewezesha vijana wengi kubakia vijijini na kushiriki shughuli za uzalishaji jambo ambalo linawapa faraja na matumaini kuendelea kuwekeza katika eneo hilo.
Massawe anasema uwekezaji wao unapokelewa kwa matokeo chanya na wananchi hali ambayo inasababisha miundombinu yao kuwa salama huku utunzaji mazingira yakionekana kuongezeka.
Meneja anasema katika kutekeleza miradi ya uzalishaji nishati jadidifu wanakutana na changamoto za mazingira, sera na kifedha.
Mfano changamoto ya kisera ni kuhusu mchakato wa kupata leseni unakuwa na mlolongo mrefu, hivyo wanaomba Serikali iangalie uwezekano wa mwekezaji kupata vibali na lesini katika kituo kimoja.
“Katika eneo la mazingira, changamoto kubwa ipo kwenye kufika maeneo husika ya kuwekeza ambayo ni magumu kufikika,” alisema.
Massawe anasema wakati wa Serikali kutoa huduma katika kituo kimoja, kuzungumza lugha moja na kuweka uwazi na kinga kwa mwekezaji ili wawekezaji waweze kuvutiwa na Tanzania.
Anasema nishati jadidifu ni nyenzo muhimu katika kutekeleza lengo la saba la SDGs la kuwepo umeme wa uhakika, bora na endelevu.
Meneja huyo anasema pia zipo changamoto za kukatika kwa umeme lakini ni kiwango kidogo tofauti na umeme wa vyanzo vya maji.
“Mufindi kuna radi ila sisi tumeweka vifaa ambavyo vinaweza kudhibiti hali hiyo isitokee, lakini pia wananchi wamekuwa walinzi wazuri pale ambapo wanaona tatizo hutoa taarifa na wao kutatau kwa wakati,” alisema.
Massawe anasema nishati jadidifu ni rafiki wa mazingira hivyo kukiwa na mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji ni wazi kuwa Tanzania itanufaika na uwekezaji huo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Akijibu swali ni kwanini hawajawekeza katika maeneo mengine kama Singida, Manyara, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Dodoma ambayo umeme wa upepo na jua unapatikana anasema mikakati yao kwa siku zijazo watawekeza katika maeneo hayo ila kwa sasa wameanza na Iringa, Mbeya na Njombe.
“Nishati tunayozalisha asilimia 85 tunauza TANESCO, asilimia 10 tumesamba vijijini na asilimia 5 tunasambaza kwenye viwanda vidogo ambavyo ni vya chai, maziwa, mbao na vingine.
“Pia tumesambaza umeme kwenye shule 44, vijiji 34, hospitali tatu, vituo vya afya 21, mashine za maji nane zinazosamba maji kwa kaya 3,000,” anasisistiza.
Anasema pamoja na kuwawezesha wananchi zaidi ya 70,000 kunufaika na nishati jadidifu kwenye kaya 5,500 hadi sasa pia wanatoa mikopo ikiwemo ya kuwauzia vifaavya kupikia vinavyotumia nishati ili kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni za kupikia hivyo kuchochea utunzaji mazingira.
“Mradi wa Uzalishaji Umeme Mwenga (MPL) pamoja na Energy for Impact + CrossBoundary/Rockefeller Foundation wamefanikiwa kutoa mikopo kati ya dola za Marekani 100 hadi dola za Marekani 1,5000 kwenye vifaa vya umeme kama mashine za kuchania mbao, za kusagia mahindi, kutotolesha, majagi na nyingine nyingi,” anasema.
Anasema kinachohitajika katika utoaji mkopo huo ni mteja kulipa asilimia 20 ya anachotaka kukopa na sehemu iliyobaki anapaswa kulipa ndani ya miezi 12 hadi 18 kwa riba ya asilimia 13.
Massawe anasema zoezi hilo la kukopesha wana kijiji limekuwa na mafanikio ambapo hadi sasa wameweza kutoa mkopo wa Sh.milioni 70 na Sh milioni imetolewa kwa vifaa vya majumbani.
“Tumepokea maombi 170 ambapo 35 kati yao ni maombi PUE na yaliyobakia ni kwa ajili ya vifaa vya majumbani kama blenda, pasi na mashine ya kupikia,” anasema.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Shirika la HakiMadin, Amani Mhinda anasema nishati jadidifu ni fursa ya maendeleo ya uchumi na jamii, hivyo Serikali inapaswa kuunga mkono wawekezaji wanaojikita huko.
Mhinda anasema nchi nyingi zimewekeza kwenye nishati jadidifu kwa kuwa ina faida nyingi ikiwemo kutunza mazingira hali ambayo inasaidia uendelevu.
“Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya nishati jadidifu tunapaswa kuwekeza katika eneo hilo ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na endelevu lakini pia eneo hilo litatupa umeme wa uhakika,” anasema.
Kwa upande wake Mhandisi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nisahati na Maji (EWURA), Victor Labaa wamejipanga kushirikiana na wadau mbalimnbali ili kuhakikisha nishati jadidifu inazalishwa nchini ili kuwezesha wananchi kupata umeme wa uhakika.
Mhandisi Labaa ametoa rai kwa wawekezaji ambao wapo tayari kuwekeza katika eneo hilo kujitokeza na EWURA itawapa ushirikiano na kuwataka watoe taarifa pale ambapo wanaona kuna vikwazo.
“Katika kuhamasisha uwekezaji wa nishati jadidifu tumetoa leseni 122 hivyo ni imani yetu hadi ifikapo 2025 lengo la Serikali kuongeza megawati 1,100 kwenye gridi ya taifa linafanikiwa,” anasema.
Mhandisi Labaa anasema miradi 63 inazalisha na 59 inasambaza ambayo inaanzia kilo wati tatu hadi 70 na inamilikiwa na watu binafsi.Miradi hiyo hadi Juni mwaka 2021 inahudumia watu 16,979 katika eneo lenye umbali wa kilomita 596.
Mhandisi wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Japhary Chinjala anasema Wizara inahamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Chinjala anasema uhamasishaji huo unaendana na wizara kuweka mazingira bora ambayo yatavutia wawekezaji kuwekeza katika nishati jadidifu ambayo inamchango mzuri katika kukuza uchumi, maendeleo na mazingira.
“Kwa sasa tuna megawati 58 zinazotokana na nishati jadidifu ambazo zinatokana na biomasia megawati 35.5, vyanzo vidogo vya maji megawati 15, umeme jua megawati 6, upepo 2.3,” anasema.