……………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga, ameshauri vikundi vya wajasiriamali kuwekeza katika kupata elimu zaidi na teknolojia ili kupata tija.
Ameyasema hayo, wakati akifungua kongamano la Vijana na Ujasiriamali liloandaliwa na Taasisi ya Tuamke Pamoja Tanzania, katika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam.
Mbunge Janeth alisema, suala la mitaji si changamoto tena kwa wajasiriamali kwani serikali inatoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia gawio la asilimia 10 linalotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
“Kikubwa wajasiriamali wekezeni katika kujifunza. Mshirikini katika mafunzo ili mtambue fursa,”alieleza Mbunge huyo.
Amebainisha, pia wajasiriamali wawekeze katika Teknolojia ambayo ndiyo msingi mkubwa katika kufikia tija kwa sasa.
“Kijana mjasiriamali unamiliki simu janja. Jiulize unaitumiaje simu hiyo katika kukuletea fursa? Pia ni lazima uwe na juhudi maarifa na uthubu,”alisema Mahawanga.
Alisema katika suala la uwezeshaji , vijana wanawake na watu wenye ulemavu mkoani Dar es Salaam, anamatarajio makubwa ya kuona matokeo chanya ili kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo.
Aliwataka wajasiriamili popote walipo kuwasiliana naye ili kusaidiana katika kufanikisha uundwaji wa vikundi, usajili wa hata kunapokuwa na mkwamo wa kupata mikopo.
“Kazi yangu mimi siyo kwenda tu Dodoma. Kazi yangu ni kuwatumikieni nyinyi wananchi. Niiteni mtaani kwenu. Siyo lazima katika ukumbi hata kwenye mikeka tutakaa. Tujadili masuala ya ujasiriamali. Nataka kuona Dar es Salaam, ikifanikiwa katika hili,”alieleza.
Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Tuamke Pamoja Tanzania, Nasra Msofe, alisema taasisi hiyo inahudumia vikundi nane vya ujasiriamali na imejikita kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana pamoja na kujitambua.
“Tunataka kuendana na sera ya serikali yetu chini ya Rais Samia ya Uchumi wa Viwanda, hivyo tumejikita katika kuhamasisha jamii kufanya ujasiriamali na kutafuta masoko ya biashara ,”alieleza.