Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akizungumza na viongozi na kamati za ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Shibula
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akikagua uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari Kisundi kata ya Bugogwa
****************************
Serikali imesisitiza uwazi, nidhamu na uadilifu katika matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi inayotokana na mpango wa maendeleo dhidi ya UVIKO-19 na na ile ya fedha zilizotokana na tozo za miamala ya simu
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitakavyo gharimu kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia tisa arobaini akiwa ameambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya ambapo amewataka watendaji na viongozi kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa kwamba hairuhusiwi kulipana posho wala kuongeza matumizi yaliyo kinyume na maelekezo ya matumizi ya fedha hizo
‘.. Tunahitaji miradi hii ikamilike kwa wakati uliokusudiwa ikiwa na ubora ule ule tunaotaka, Ni bora tukapunguza matumizi kwa shughuli ambazo tunaona zinaweza zikafanywa na jamii badala ya kulipa watu wakafanya shughuli hizo kuliko kuongeza matumizi ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala mbali na kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa vyumba vya madarasa amesisitiza umakini katika suala la ulipaji wa mafundi, ununuzi wa vifaa sambamba na kuelekeza kutoingiwa kwa mkataba wa jumla katika uendeshaji wa shughuli za ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ili kuepuka kukwama kwa kazi pindi fundi wa mradi anapopata dharula ikiwemo kuumwa, uzembe au sababu nyenginezo
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amefafanua kuwa yapo maelekezo na hatua mbalimbali ambayo yamekwishatolewa juu ya utekelezaji wa mradi huo ili kuongeza ufanisi na ubora wake ikiwemo ununuzi wa pamoja wa baadhi ya vifaa sambamba na kusisitiza umakini na uzingatiaji wa maelekezo ya Serikali na viongozi wake katika kutekeleza miradi hiyo
Nae Diwani wa kata ya Shibula Mhe Swila Dede ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwa uamuzi wake wa kutembelea na kukagua hatua za ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa kwani kitendo hicho kitasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazotokana na ufahamu mdogo wa maelekezo ya Serikali kwa baadhi ya watumishi na viongozi wa ngazi za chini juu ya sheria, taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha za ujenzi sambamba na kuongeza ari na morali ya ushiriki wa jamii katika kujitolea nguvu na mali kukamilisha ujenzi huo
Katika ziara hiyo shule ya sekondari Sangabuye, Bugogwa, Kisundi, Shibula na Lumala zilitembelewa