******************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya chama cha mapinduzi (CCM) mkoani Njombe ya kukagua uhai wa chama hicho ambayo hufanywa na Sekretarieti ya chama hicho ngazi ya mkoa sekretarieti hiyo imewasili wilayani Ludewa na kuzungumza na sekretarieti zote za kata 26 zilizopo wilayani humo sambamba na madiwani wa kata hizo.
Masafara huo ukiongozwa na katibu wa chama hicho ngazi ya mkoa Amina Himbo amewataka viongozi hao kuongeza juhudi katika usajili wa wanachama katika mfumo wa kielektroniki sambamba na kutimiza wajibu wao kama wananchama.
Amesema viongozi walio wengi wamekuwa wakisubiri wakati wa uchaguzi ndipo waanze kutafuta wanachama wa kuwasajili kitu ambacho si sahihi kwani wanapaswa kufanya shughuli hizo wakati wote kwani uhai wa chama ni kuwa na wanachama wengi wanaolipa ada na hasa wanachama wapya.
Sanjali na hilo katibu huyo amewataka makatibu wa CCM katika kata zote kuhakikisha wanasimamia vyema miradi ya chama iliyopo katika chama hasa katika majengo ambayo wameyapangisha.
“Mali za chama zinapaswa kusimamiwa vyema ili tuweze kuinua uchumi katika chama chetu, kwa wale wenye miradi ya majengo ambayo mmepangisha hakikisheni wapangaji wanalipa kodi ya pango kwa kutumia ‘control number’ na si kupokea mkononi maana hiyo haita hesabika kama imelipwa”, amesema Bi. Himbo.
Baada ya kuzungumza na sekretarieti hizo pamoja na madiwani viongozi hao walitembelea wanachama wa shina namba 12 lililopo katika kitongoji cha Ibani ambapo katibu siasa na uenezi wa mkoa huo Erasto Ngole alitoa elimu juu ya majukumu pamoja na umuhimu wa mabalozi.
Amesema mabalozi wana umuhimu mkubwa katika chama kuliko kiongozi yeyote wa chama kwani uhai wa chama huanzia ngazi ya chini kwenda juu hivyo mabalozi wana nafasi kubwa katika chama na wanapaswa kuwekwa katika hali ya umuhimu wao .
Ameongeza kuwa viongozi hao wa mashina wanapaswa kufanya vikao mara kwa mara ili kujadili masuala mbalimbali juu ya uhai wa chama sambamba na kuona njia za kuongeza wanachama.
“Mabalozi ni watu muhimu sana katika chama, uhai wa chama cha mapinduzi unaanzia katika mashina na uhai huu unakuwepo endapo viongozi hawa wa mashina watafanya mikutano mikuu ipasavyo”, Amesema Ngole.
Amesema mikutano hii mikuu itakayoandaliwa na mwenyekiti wa kitongoji inatakiwa kuanza na agenda kuu ya uhai wa chama kisha inafuata ulinzi na usalama na baada ya hapo zitafuata agenda nyinginezo ambazo zitakuwa zimeandaliwa huku akiwataka viongozi ngazi ya kata na wilaya kuhudhuria mikutano hiyo ya mabalozi.