……………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amesema Serikali inatarajia kutekeleza miradi 218 ya maji katika halmashauri mbalimbali hapa nchini kupitia fedha za UVIKO 19 ambazo ni takribani Trioni 1.3 ambapo Wizara ya maji imepata mgao wa shilingi bilioni 139.4.
Akizungumza na Watendaji wa Wizara ya Maji, wakurugenzi wa mamlaka mbalimbali za maji na wasambazaji na watengenezaji wa vifaa vya ujenzi hapa nchini ambapo amesema miradi hiyo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 104 na miradi mingi itatekelezwa vijijini na michache mijini.
“Katika miradi hiyo 218 takribani miradi 172 ni miradi ya vijijini na takribani 48 itakuwa ya mijini ambapo huko hakuna shida kubwa ya maji na ninawataka miradi hii ikamilike kwa wakati na kwa ubora” amesema Eng. Sanga.
Aidha eng. Sanga amebainisha kuwa kati ya fedha hizo takribani bilioni 17.5 kati ya bilioni 139.4 zitatumika katika kununua mitambo 25 za uchimbaji wa visima na mitambo hiyo itasambazwa kila mkoa hapa nchini kurahisisha shughuli za uchimbaji visima.
“Sasa hapa mtaona mitambo 25 lakini mikoa ipo 26 hapa tuna mitambo 8 kutoka DDCA sasa hapo mtambo mmoja utaupeleka mikoani na saba iliyobaki hii itakuwa ikisaidia kuongeza nguvu katika mikoa yenye changamoto kubwa zaidi” amesema.
Sambamba na hilo amebainisha kuwa Wizara imepanga kununua seti nne za mitambo maalumu ya kupima maji ardhini ili kuondoa kadhia ya mda mrefu ambapo serikali ilikuwa ikitumia fedha nyingi katika kuchimba visima lakini maji yanakuwa hamna na sasa ukichimba visima itakuwa uhakika.
Pia amebainisha kuwa watatumia zaidi ya bilioni 17 katika kununua mitambo ya kisasa seti 5 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa mabwawa hapa nchini ambayo yatatumika katika shughuli mbalimbali ikiwa katika kuhifadhi maji kwa matumizi na katika kilimo cha kisasa.
Aidha eng. Sanga amewataka watendaji watakaokwenda kutekeleza miradi hiyo kuhakikisha kila mradi unakuwa na jarida lake litakalokuwa na taarifa zote kuanzia mwanzo wa mradi hadi mwisho ili iwe rahisi katika kufuatilia miradi hiyo na kusisitiza ushirikishwaji katika ngazi zote.
Pia ameagiza kuhakikisha watendaji watakaotekeleza miradi hiyo kuwashirikisha viongozi wa maeneo hayo kuanzia mkoa hadi ngazi ya mtaa pia kuwashirikisha Wabunge, Madiwani kwani wao ndio wanaojua sehemu sahihi za kutekeleza miradi hiyo na maeneo yenye changamoto zaidi za maji.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji mhandisi Nadhifa Kemikimba amewataka wataalamu wa maji katika maeneo yao kufanya tathmini pia kuongeza kasi kwani imebaki miaka mitatu kufikia mwaka 2025 ambapo lengo la Wizara ni kufikia asilimia 95 mijini na asilimia 85 maeneo ya vijijini.