Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Prof
Adolf Mkenda tarehe 28 Octoba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Bi
Kate Somvongsiri katika Ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo
wamejadili kwa kina kuhusu vipaombele vya serikali katika wizara ya kilimo.
Pia wamejadili umuhimu wa
kutatua tija na uzalishaji mdogo kwenye mazao ya wakulima ili kutafuta
muarobaini wa kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
Kadhalika wamejadili umuhimu
wa kuongeza nguvu na umuhimu katika sekta ya utafiti ili kubaini nini
kinahitajika katika ardhi ya kilimo katika maeneo mbalimbali ya wakulima nchini
ili wakulima waweze kutambua mazao yanayokubalika katika maeneo yao pamoja na
kutambua aina na kiasi cha mbolea kinachohitajika.
Vilevile majadiliano hayo
yamejikita Zaidi kuhusu umuhimu wa kuboresha huduma za ugani, ambapo Waziri
Mkenda ameeleza kuwa tayari wizara yake imeanza kuchukua hatua madhubuti ikiwa
ni pamoja na kuwawezesha maafisa ugani kuwa na Pikipiki ambazo zitawarahisishia
kuwafikia wakulima kwa wakati.
Aidha, katika mazungumzo hayo
wamejadili umuhimu wa Ugharamiaji wa kilimo (Agro Financing), pamoja na
kuwekeza kwenye Kilimo Anga.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID Bi
Kate Somvongsiri amemueleza mwenyeji wake Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf
Mkenda kuwa USAID dhamira ya kushiriki katika kikao kazi hicho ni pamoja na
kukutana nae ili kujitambulisha kwake kujua vipaombele vya Wizara na kuandaa
mkakati wa namna ya kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za
Kilimo.