Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (hayupo pichani) jana ambapo kilihusu kuwakumbusha majukumu yao ya kusimamia miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe.Joseph Mkirikiti akizungumza na Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata jana Sumbawanga ambapo amewataka kwenda kuhamasisha zoezi la chanjo ya UVIKO-19 na maandalizi ya sensa ya watu na makazi kwa kuwaelimisha wananchi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akitoa mada kuhusu chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata za mkoa wa Rukwa ili wakashiriki kuelimisha wananchi kikao kilichofanyika jana Sumbawanga.
………………………………………………………………….
Maafisa Watendaji wa Kata pamoja na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Rukwa wametakiwa kutambua kuwa wanalo jukumu la kusimamia ukusanyaji na matumizi ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwenye halmashauri.
“Mnatakiwa kutambua kiasi cha fedha za mapato ya ndani zinazokusanywa kutoka kwenye vijiji, mitaa na maeneo ndani ya kata na tarafa zenu kwenda kwenye halmashauri ili mtoe usimamizi wa karibu wa matumizi kwenye miradi ya maendeleo” alisema Mkirikiti.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa maelekezo hayo jana (28.10.2021) wakati alipofanya mkutano na Maafisa Tarafa wote wa mkoa wa Rukwa na Maafisa Watendaji wa Kata mjini Sumbawanga na kuwasisitiza kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha toka kwa vyanzo mbalimbali.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kusema watendeji hao wa serikali wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanafuatilia fedha zinazopelekwa kwenye maeneo yao toka serikali kuu kutekeleza miradi ya shule,afya,miundombinu,maji hifadhi za mazingira nk.
Aidha, alitoa maagizo mengine manne kwa watendaji hao ,kwanza kwenda kutambua miradi yote inayotekelezwa kwenye kata na tarafa zao ili waisimamie ikamilike kwa wakati na ubora.
Pili, kutatua migogoro ya wananchi kwa kuwatembelea na kusuluhisha katika ngazi za vijiji na mitaa badala ya kusubiri viongozi ngazi ya wilaya au mkoa na tatu, kusimamia utunzaji wa mazingira ikiwemo kuhamasisha wananchi kupanda miti na kudhibiti uchomaji moto misitu.
“Mkoa huu wa Rukwa miti inakatwa ovyo, moto kichaa, uchomaji mkaa usiofuata taratibu. Hili nendeni mkalisimamie kwa karibu” alisisitiza Mkirikiti
Agizo la nne amewataka watendaji hao wa kata na tarafa kuelimisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa korona na pia kuhamasisha wananchi kujiandaa kwa zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu, aliwataka watendaji hao kuwa mstari wa mbele kwa wao binafsi kuchanja kisha kuhamasisha wale ambao bado hajawachanja.
“Nawaomba sisi watendaji wa serikali tuwe mstari wa mbele kuuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujitokeza kuchanja na kuwaelimisha wenzetu, chanjo ni salama na inasaidia kupunguza maambukizi na pia kuzuia vifo vitokanavyo na ugonjwa wa korona” alisema Dkt. Kasululu.
Dkt. Kasululu aliongeza kusema mkoa umepokea dozi 24,183 za chanjo ya UVIKO-19 awamu ya pili aina ya Sinopharm ambapo kazi ya kuhamasisha wananchi imeanza hivyo amewataka watendaji hao kushiriki kwenye zoezi hilo pamoja na wataalam wa afya kwenye maeneo yao.
Naye Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Sabina Songela akitoa mada kuhusu majukumu na wajibu wa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata alisema wanalo jukumu la kusimamia suala la upatikanaji huduma kwa wananchi ili kuleta ustawi na amani kwenye maeneo yao.
Mkutano huo wa Maafisa Tarafa toka tarafa zote 19 za Mkoa wa Rukwa na Maafisa Watendaji Kata toka kata 20 za Manispaa ya Sumbawanga ni kwanza tangu Mkuu huyo wa Mkoa alipoteuliwa kuongoza mkoa wa Rukwa hapo mwezi Mei mwaka huu na ulilenga kuwakumbusha wajibu wao kwenye utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Mwisho.
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
SUMBAWANGA
29.10.2021