******************************
Na Mwandishi Wetu, Kibaha Pwani.
MAMLAKA ya Dawa na vifaa Tiba [TMDA] mapema leo tarehe 29 Oktoba 2021 imezindua rasmi Kamati ya Wajumbe wapya wa Kitaalamu wa Usalama wa Dawa, Chanjo na bidhaa zingine zikiwemo vitendanishi na tumbaku ambapo kamati hiyo ni ya tano [5] tangu Mamlaka hiyo ianzishwe na ina Wajumbe wapya wenye jukumu la kuhakikisha kwamba masuala ya usalama wa bidhaa husika yanazingatiwa kwa mujibu wa vigezo vya kitaifa na Kimataifa ili kulinda afya ya mlaji.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika mjini hapa katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wauguzi na Wakunga, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Yonah Mwalwisi, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo, alisema Wajumbe hao wapya wanajukumu kubwa la kusaidia Mamlaka hiyo hapa nchini ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.
‘’Niwapongeze kwa wale wajumbe wapya mliochaguliwa kwenye kamati hii mpya ambayo ni ya Tano tangu Mamlaka ianzishwe. Lakini pia nizipongeze kamati zote zilizopita kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika ili kulinda afya ya Watanzania.
Kamati hii huundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219 ikiwa na jukumu kubwa la kuishauri na kuisaidia Mamlaka katika kuzingatia masuala ya usalama wa bidhaa zinazodhibitiwa na Mamlaka hapa nchini ’’ alisema Dkt. Mwalwisi.
Kamati hiyo ina wataalamu waliobobea katika tasnia ya dawa na vifaa tiba ambao ni maprofesa, madaktari bingwa na wataalam wa tasnina ya dawa waliobobea ambapo idadi ya ni wajumbe 16 ambapo watadumu kwa muda wa miaka mitatu.
Dkt. Mwalwisi alisema kuwa, Kamati hiyo mpya ni muhimu sana katika kuhakikisha mifumo yote ya kufuatilia usalama wa bidhaa zinazodhibitiwa inaimarishwa, taarifa za maudhi ama madhara zinapatikana kwa wakati na kufanyiwa tathmini ya kina na hatimaye kusaidia kutoa maamuzi mbalimbali katika kulinda afya ya jamii kwa kuzuia yasitokee kabisa au kuyapunguza.
‘’Tunatambua kwamba matumizi ya bidhaa za tiba yameongezeka sana kutokana na uwepo wa ugonjwa wa UVIKO-19 na magonjwa mengine duniani.
Wananchi wanatumia bidhaa za tiba hususani dawa nyingi kwa wakati mmoja bila kupata ushauri wa wataalam.
‘’Hata chanjo za UVIKO-19 ni ngeni kwa Taifa letu la Tanzania na kwa dunia nzima. Hali hii inaweza kusabanisha wananchi kupata maudhi mbalimbali. Hivyo ni lazima TMDA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kuimarisha mifumo iliyopo ya kufuatilia usalama wa bidhaa za tiba.
“Ni tegemeo langu kwamba kamati hii itasaidia sana katika kuhakikisha mifumo ya ufuatiliaji inaimarika zaidi alisema.’’ Alisema Dkt. Mwalwisi.
Dkt. Mwalwisi alisema kuwa, pamoja na kwamba utaratibu wa kufuatilia usalama wa dawa, chanjo kwenye soko ulianza tangu kuanzishwa kwa TMDA (iliyokuwa TFDA) mwaka 2003 na imeendelea kufanyika hadi sasa.
‘’Takwimu zinaonyesha kuwa bado mwamko wa wataalam wa afya na wananchi kwa ujumla katika kutoa taarifa juu ya madhara ya bidhaa tiba ni mdogo na hivyo taarifa chache zinafika TMDA ikiwa ni wastani wa ripoti 6,000 hadi 8,000 kwa mwaka.
Aidha, pamoja na kupokea taarifa hizo, bado taarifa hizo zinakuwa hazina ubora au kukosa baadhi ya taarifa muhimu zinazosaidia kufanya tathmini ya kina kuhusu uhusiano uliopo kati ya dawa au bidhaa inayohisiwa kuleta madhara na madhara yaliyotokea kitaalam tunaita ‘causality assessment’.’’ Alisema Dkt. Mwalwisi.
‘’Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na idadi inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kukusanya angalau ripoti 200 kwa wakazi (inhabitants) milioni 1 kwa mwaka. Hivyo kwa idadi ya watu milioni 60 walioko katika nchi yetu, inatakiwa tuwe tunakusanya ripoti 12,000 kila mwaka ili kutoa uthibitisho wa kisayansi (evidence) juu ya usalama wa bidhaa tiba na kuchukua hatua stahiki.’’ Alisema Dkt. Mwalwisi.
Dkt. Mwalwisi aliongeza kuwa, kutokana na idadi hiyo ndogo ambayo haifikii kiwango kinachohitajika, TMDA imekuwa ikifanya mafunzo na uhamasishaji mara kwa mara ili kuwakumbusha watendaji na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa za madhara ya dawa, chanjo na vifaa tiba
hatua hii inasaidia kufahamu aina bidhaa tiba zinazoleta madhara, madhara yenyewe na watu wanaoathirika zaidi na taarifa hizo kusaidia kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuziondoa kwenye soko, kusitisha matumizi, kubadilisha matumizi ya dawa au chanjo.
‘’Kuanzia tarehe 25 hadi leo 28 Oktoba, 2021 mmepata mafunzo ya kuwawezesha kuifanya kazi hii vizuri na kuwa na uelewa wa majukumu yenu kama wajumbe wa kamati ya usalama wa bidhaa za dawa na chanjo.
Ni matumaini ya TMDA kwamba baada ya mafunzo hayo, mtaweza kuifanya kazi yenu kwa utaalamu mlionao na kwa weledi zaidi na kuweza kuishauri Mamlaka vizuri zaidi mkiendeleza pale ambapo kamati zilizopita zilitufikisha.’’alisema.
Aidha, Dkt. Mwalwisi aliishukuru sana Kamati iliyomaliza muda wake kwa kufanya kazi nzuri ya kufikisha katika hatua iliyopo sasa ambapo taarifa zikaweza kuongezeka kutoka 300 hadi wastani wa 6,000 hadi 8,000 kwa mwaka.
‘’Ni matarajio yangu kwamba Kamati hii inayoanza majukumu yake leo, itafanya kazi vizuri zaidi na hatimaye tuweze kufikia malengo yaliyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, ni matarajio yangu kwamba mtafanya utekelezaji wa majukumu yenu kwa mujibu wa Kanuni za Usalama wa Dawa, miongozo iliyopo na hadidu rejea za Kamati.
Nichukue nafasi hii pia kuishukuru sana Taasisi isiyo ya Kiserikali MTaPs – MSH kwa msaada wa kifedha na kuwezesha mafunzo kwa wajumbe wapya wa kamati na utekelezaji wa uzinduzi wa kikao cha Kamati hii vilevile nashukuru kwa kuweza kutupatia ushauri wa kitaalam.’’ Alimalizia Dkt. Mwalwisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa miradi wa programu ya dawa, ufundi na huduma za maabara kutoka [MSH] iliyochini ya Shirika la Kimataifa la USAID kupitia mradi wa [MTaPS], Dkt. Edger Lusaya wao kama wadau wameweza kutoa msaada wa kifedha wa kuweza kuandaa na kuwezesha mafunzo hayo kufanyika ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha afya ya wananchi wake.