******************************
Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Msasani imefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo, inayoongozwa na Diwani Luca Neghesti @lneghesti ambapo walifanikiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza nasi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Msasani, Nyerere Mnyupe amesema kuwa wamekagua miundombinu, afya, elimu na mazingira kwa ujumla na hivyo kuridhishwa na utekelezaji uliyofanywa chini ya Diwani huyo.
“Tumekagua madarasa ya shule ya sekondari Oyster bay ambayo yamejengwa kwa kipindi hiki cha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi tumeridhika na gharama na ujenzi bora. Tumepita kukagua nyumba ya waalimu ambayo imefanyiwa ukarabati na ujenzi unaendelea, unaridhisha. Tumekwenda Bonde la Mpunga na Mikoroshoni tumeangalia ujenzi ambao diwani kwa weledi wake, juhudi zake na ubunifu wake yeye mwenyewe ametengeza makaravati na mifereji kwaajili ya kupitisha maji.”- amesema Nyerere Mnyupe Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Msasani
Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Msasani, Badili Mangula ameongeza kuwa ”Tumefanya ziara katika maeneo mbalimbali ambapo kwa kiasi kikubwa tumeona utekelezaji wake. Tunachukua fursa hii kumshukuru Mhe. Luca Neghesti Diwani wa Kata kwa jinsi anavyojitahidi kufanya kazi vizuri, huko akishirikiana na Chama Cha Mapinduzi.”
Baadhi ya miradi iliotembelewa ni pamoja na:
1. Uzio wa Zahanati ya Kata
2. Mfereji wa maji ya mvua mtaa wa Mikoroshoni
3. Daraja la karavati Kwa Kusila, mtaa wa Bonde la Mpunga
4. Daraja la karavati Kidongo, mtaa wa Bonde la Mpunga
5. Barabara ya lami Ghuba road/Peninsula Hospitali
6. Shule ya Msingi Msasani A ukarabati wa sakafu katika madarasa
7. Ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kata
8. Ukarabati nyumba za waalimu katika shule ya msingi Oyster Bay
9. Ujenzi wa madarasa mapya 6 katika shule ya sekondari Oyster Bay
10. Ukarabati madarasa 6 kupauliwa na 3 kujenga sakafu katika shule ya sekondari Oyster Bay