****************************
Na Mwandishi Wetu
Diwani wa Kata ya Kivukoni, Ilala, Dar es Salaam, Sharik Choughle, amekabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 10.5 kwa Kikundi cha Wanawake cha Upendo Ferry.
Fedha hizo zimetolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kupitia mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri kwaajili ya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akikabidhi mfano huo wa hundi, Diwani Choughle alikitaka kikundi hicho kuzitumia kwa malengo yaliyo kusudiwa ili kuinua kipato .
“Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza halmashauri ziendelee kutoa fedha hizi ambazo zinatokana na asilimia 10 ya pato la ndani la halmashauri. Asilimia nne inaenda kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu. Leo Upendo Ferry mmepata tunamshukuru sana Rais Samia,”alisema.
Pia alivitaka vikundi vyote vilivyo nufaika na mkopo wa fedha hizo kurejesha kwa wakati ili kuvipa fursa vikundi vingine kukopa.
Nao wana kikundi hicho walimshukuru diwani huyo kwa kusimamia kikamilifu upatikanaji wa mkopo huo .
“Diwani ametupigania na tumepata. Lakini kubwa zaidi ni kwa Rais Samia ambaye yuko mstari wa mbele kuhakikisha mikopo hii inaendelea kutolewa. Tunashukuru pia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kuhakikisha fedha hizi zinaendelea kutengwa na kutolewa,”alisema Sada Rajabu.
Zakia Abdallah alisema, kikundi chao ni cha mama lishe na kwamba mkopo wao huo utawasaidia kukuza mitaji yao.