Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli (mwenye overall) akishiriki kuchimba msingi wa madarasa katika Kata ya Isandula mjini Magu.
Akinamama wa Kijiji cha Kahangara wakishiriki kuchimba msingi wa darasa jana katik eneo l Shule ya Sekondari Kahangara,katikati yao aliyevaa overall ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akishiriki kuchimba msingi wa mdarasa na kuopoa udongo huku wananchi wakishudia jana.
Wananchi wa Nyanguge wamkisiliza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli (wa pili kutoka kushoto), baada ya kushiriki zoezi la kuchimba msingi wa mdarasa sita ya shule ya sekondari Nyanguge jana.Kushoto wa kwanza ni diwani wa kata hiyo, Elisha Hilal.Picha na Baltazar Mashaka
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
WANANCHI zaidi ya 2,000 wa vijiji vya kata za Kahangara,Nyanguge na Isandula wilayani Magu,jana wamekatisha usingizi kwenda kumwuunga mkono, Rais Samia Suluhu Hassan,kuchimba misingi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Wananchi hao wa kada mbalimbali (wazee,wanawake na vijana) walijitokeza kwenye maeneo ya miradi hiyo majira ya saa 12 alfajiri wakiungana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Salum Kalli kuchimba misingi 21 kwa nguvu zao na hivyo kuokoa sh.milioni 4.2 endapo ingechimbwa na wakandarasi.
Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wenzao, Abel John Magashi wa Kijiji cha Bundilya,Kata ya Kahangara na Aloyce Machombo,mkazi wa Kijiji cha Muda, Kata ya Nyanguge,kwa nyakati tofauti walisema mwitikio wao unauunga mkono juhudi za Rais Samia,kuwaletea fedha za ujenzi wa madarasa katika kukabiliana na upungufu uliopoi li kuondoa msongamano wa wanafunzi.
“Wananchi wa Kahangara tunamshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za madarasa,sisi kwa uchumi wetu duni tusingeweza kujenga madarasa 10 kwa wakati mmoja,pia mkuu wa wilaya yetu kwa kushiriki na kutuhamasisha kuchimba msingi ili kuongeza madarasa sababu yaliyopo ni machache na hayakidhi mahitaji,”alisema Magashi.
Naye mkazi wa Kijiji cha Muda na Mwenyekiti Bodi ya Shule ya Sekondari Nyanguge,Machombo alisema Rais baada ya madarasa kukamilika aendelee kuwasaidia fedha wajenge uzio wa shule ili kuimarisha taaluma,usalama na kuepusha uvamizi wa eneo la shule unaofanywa na jamii ambapo shule ina wanafunzi 1,368 wasichana 720,ina upungufu wa vyumba 44 na vilivyopo ni 14 tu.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake,Mary Shija wa Kijiji cha Bugumangalo,alisema serikali kwa kutoa fedha kujenga madarasa itasaidia kukuza taaluma,kuongeza ufaulu,kuondoa msomangamano wa watoto na kuwaepusha na maradhi ya mfumo wa hewa.
“Fedha hizo zina mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu na taaluma kwa watoto wetu,watasoma kwa uhuru na walimu watafundisha kwa raha,ndiyo maana tumeshiriki kuchimba msingi wa madarasa ili kumwunga mkono Rais Samia,ahsante sana mama kwa kuguswa na changamoto ya watoto wetu,”alisema.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Magu,Kalli,baada ya kushiriki kuchimba msingi katika Shule ya Sekondari Kahangara,alisema serikali imetoa sh. bilioni 2.464 kujenga vyumba 123 vya madarasa na kuwataka wasikubali kugawanywa,kuyumbishwa wala kurubuniwa na watu wanaopinga na kuzuia maendeleo.
“Asitokee mtu wa kuwagawa kwenye suala la maendeleo na kuleta chokochoko kwa maslahi binafsi,kushiriki kwenu kuchimba misingi 10 ya madarasa na kuikamilisha leo,mmeokoa sh. milioni 2 ambazo zitatumika kuanzisha ujenzi wa hosteli ili kuwanusuru watoto wa kike na kuwapunguzia umbali mrefu wa kwenda shule na kurudi nyumbani,”alisema.
Kalli alisema wananchi wa Kata ya Kahangara na vijiji vyake wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa upendeleo uliowawezesha kupata fedha nyingi kuliko kata zingine,fedha ambazo zimetokana na mapambano ya Uviko-19 na mwitikio wao huo ni dalili wanaunga mkono juhudi za Rais kutatua changamoto za elimu.
“CCM ndio wenye ilani inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita, fedha ipo na kazi yenu ni nguvu kazi mnayoifanya hapa wala mtu asiwafanyie ghiliba na kuwazunguka ili kukwamisha maendeleo,chenchi ya fedha zitakazookolewa zitafanya kazi zingine,niwapongeze kwa kukatisha usingizi wenu kuja kuchimba misingi ya madarasa,”alisema Kalli.
Mkuu huyo wa Wilaya alisistiza kazi nzuri iliyofanywa na wananchi hao wa Kijiji cha Kahangara,atasimamia yapatikane mabati ya kuezeka zahanati ya kijiji hicho wapate huduma za matibabu karibu na kuahidi kusimamia chenchi ya fedha za madarasa zijenge hosteli ya wasichana ambapo atatafuta fedha za kuiezeka.
Akiwa Nyanguge sekondari Kalli alisema heshima waliyopewa wananchi wa Magu na serikali kazi yao ni nguvu kazi ya kuchimba misingi ya madarasa ili kupunguza gharama na kuonya chenchi itakayobaki haitachakachuliwa na mtu,itabaki shuleni ili waamue fedha hizo zifanye nini.
Alisema wana mkakati wa kuifanya Shule ya Sekondari Nyanguge kuwa na hadhi ya elimu ya juu kwa kuanzisha kidato cha tano na sita kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Diwani wa Kata ya Nyanguge (CCM),Elisha Hilal,aliwaambia wananchi wa kata hiyo kuwa maendeleo yao watayaleta kwa nguvu zao, na madarasa hayo sita yatapunguza baadhi ya changamoto yatakapokamilika ambapo ufaulu wa watoto kwenye shule hiyo ni mzuri ingawa imezidiwa wingi wa wanafunzi na kuwataka kujiandaa kujenga nyingine ya pili.