Na Joseph Lyimo
MTOTO wa kike wa jamii ya kifugaji bado hapewi kipaumbele katika
kupata elimu hivyo mara nyingi huishia kuolewa wakiwa wadogo na
kutokana na mfumo dume uliopo wanashindwa kupinga hivyo ndoto zao
mbalimbali hukatizwa wakiwa na umri mdogo.
Hata hivyo, hivi sasa kwenye jamii ya kifugaji ya kimasai ambao
wanapatikana Tanzania nzima ila mikoa ya kanda ya kaskazini ndiyo
nyumbani kwao wamebadilika kwa kusomesha watoto.
Wilaya za Simanjiro, Kiteto mkoani Manyara, wilaya za Arumeru,
Longido, Arusha Ngorongoro na Monduli, mkoani Arusha, wasichana wa
jamii ya kifugaji wamepatiwa elimu japokuwa mwamko siyo mkubwa sana.
Diwani mstaafu wa kata ya Oljoro Namba tano, wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, Mathayo Lormuje anasema yeye ni miongoni mwa wafugaji
wanaojali elimu kwani amewasomesha Watoto saba wakike watatu na
wakiume wanne bila kubagua.
Lormuje anasema hivi sasa watoto hao saba wote wamehitimu vyuo vikuu
na anatarajia kuwasomesha wengine watatu waliobaki ili kutimia watoto
10.
Amesema watoto wake wamehitimu shahada mbalimbali ikiwemo sheria,
udaktari, ufamasia, ualimu na maendeleo ya jamii hivyo elimu hiyo
itawanufaisha watoto hao na jamii ya eneo hilo kwa ujumla.
“Namshukuru Mungu kwa sababu wake zangu watatu wa jamii ya kimasai
walinipa moyo kama wapiganaji wa kutaka watoto wao wapate elimu,”
amesema Lormuje.
Amesema watoto hao wamekuwa wanamtia moyo kwani alikuwa anauza mifugo
kwa lengo la kuwasomesha watoto wakike na wao hawajamwangusha.
Ametoa ombi kwa shule za sekondari za wilaya ya Simanjiro isiwe na
sura ya kata ila ziwe na sura za bweni ili watoto wa jamii ya kifugaji
waweze kusoma kwa urahisi.
“Watoto wengi wa jamii ya kifugaji wanashindwa kusoma kutokana na
umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni ila wakiwa wanasoma na kulala
kwenye mabweni watapenda elimu,” amesema Lormuje.
Amesema maeneo mengi ya wafugaji kutoka majumbani hadi shuleni ni
mwendo mrefu hivyo siyo kazi rahisi kwa mtoto miaka 14 kushuka chini
kutembea umbali wa kilometa 10 na kurudi kilomita 10 kwa kila siku.
Mkazi wa kijiji cha Namalulu kata ya Naberera Julius Mollel amesema
kitendo cha kuwasomesha watoto wa kike hivi sasa ni chakupongezwa
kwani jamii hiyo inazidi kupiga hatua kwa kubadili mtazamo wa watoto
wa kike.
Mollel amesema hata watu wengine wataona wivu kuona mzee Lormuje
amefanikiwa kuwasomesha Watoto wake wa kike na hivyo wataiga jambo
hilo zuri kwa lengo la kuwanufaisha watu wa jamii hiyo.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Alhaji Batenga amesema
kujenga mabweni kwenye wilaya hiyo kutakuwa chachu ya watoto wa
kifugaji kupata elimu.
“Suala la kujenga mabweni kwenye shule zenye changamoto ya umbali
halina mjadala hivyo tunapaswa kuhakikisha tunalitimiza hilo kwa
kujenga mabweni ili watoto wasome wakiwa shuleni,” amesema Batenga.
Hata hivyo, Batenga amesema pamoja na shule za bweni bado jamii ya
wafugaji inamwamko mdogo wa kutoa chakula shuleni ili wanafunzi hao
wale chakula shuleni.
“Mwitiko wa wazazi kuchangia chakula kwenye shule za msingi bado ni
mdogo kwani endapo wangeunga mkono serikali na kuchangia chakula
wanafunzi wengi wangenufaika,”.
Ofisa elimu ya msingi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus
Tairo amesema shule za bweni zitachangia kwa kiasi kikubwa kunyanyua
kiwango cha elimu kwenye eneo hilo.
Tairo amesema kwenye wilaya ya Simanjiro kuna shule tatu za msingi za
bweni ambazo wanafunzi wanalala shuleni na kusoma kwenye shule hizo.
Amezitaja shule hizo zenye mabweni kuwa ni shule ya msingi Naberera
iliyopo kata ya Naberera, shuel ya msingi Ruvu Remit iliyopo kwenye
kata ya Ruvu Remiti na shule ya msingi Simanjiro iliyopo kata ya
Emboreet.
Diwani wa kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro Taiko Kurian Laizer
anasema mtoto wa kike anapaswa kupewa elimu kama mtoto wa kiume kwani
hivi sasa hakuna ubaguzi wa mtoto kwa jamii ya kifugaji.
Taiko anasema kwenye maisha yake anamkumbuka marehemu Reginald Mengi
ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini aliyejitolea kuwasomesha
watoto 27 wa jamii ya kimasai hadi nje ya nchi.
“Marehemu Mengi alinipa moyo wa kupenda kusomesha Watoto wa kike
kutokana na kitendo hicho na bado nitamkumbuka milelel kwa kujali
jamii yetu ya wafugaji wa kimasai na aliwaasa hao watoto kuwa wasome
kisha warudi kusaidia nyumbani,” amesema Taiko.