…………………………………………….
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wamelalamikia kampeni ya kuhamasisha wanaume kufanyiwa tohara kwa madai kuwa kampeni hiyo inalazimisha wanaume kufanya tohara na si tendo la hiari
Wakizungumza katika kikao cha kwanza cha Baraza la madiwani cha mwaka 2021/22 madiwani hao wamedai kuwa kampeni hiyo inahatarisha ndoa za watu
‘Kwakweli kampeni hii inafedhehesha, unakuta mabinti wanaambiwa ukimkuta mwanaume ana mkono wa sweta mkatalie, sasa hivi tutafika kweli?’ alisema diwani wa kata Mwamkulu Kalipi Katani
Aidha alishauri kuwa kampeni hiyo iwahusu vijana na watu walio chini ya umri wa miaka hamsini na kutaka wawepo na watu wazima wanaotoa huduma hiyo ya tohara
Akipinga hoja hiyo Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Ukimwi Crissant Mwanawima ambaye ni diwani wa kata ya Kasokola alisema madiwani hawana budi kukubaliana na wataalamu kwani tohara ina manufaa makubwa
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa Dr. Limbu Mazoya amekiri kuwepo kwa kampeni hiyo ambapo amesema faida mojawapo ya tohara ni usafi wa uhakika, pili tohara ni kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 40% sanjari na kumkinga mwanamke na saratania ya shingo ya kizazi.
Dk. Limbu amesema ni kweli wanawahamasisha wanawake kuwakataa wanaume ambao hawajafanyiwa tohara kwa lengo mahsusi la kuhamasisha jamii kuona suala la tohara ni la msingi
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumri amewataka madiwani kutokupingana na wataalamu
‘ Ifike mahali tuukubali tu ukweli, huwezi ukalazimisha daktari wa tohara awe mzee linapofika suala la afya huwezi kuchagua daktari, alisema Sumri