****************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba amesema miradi mbalimbali ya kimaendeleo inatarajiwa kutekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Warioba ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Amesema miradi mbalimbali ya kimaendeleo itafanikishwa kupitia fedha hizo zilizotolewa na Serikali.
Amesema mji mdogo wa Mirerani wenye kata mbili za Mirerani na Endiamtu zina wakazi wengi hivyo inatakiwa kujengwa kituo kipya cha afya kwenye kata ya Mirerani ambayo haina kituo cha afya.
“Ila kituo hicho cha afya kipya kinapaswa kujengwa kipya kikiwa na eneo na kuchimbwa msingi na siyo kupandisha hadhi zahanati,” amesema Warioba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Baraka Kanunga amewataka madiwani wa kata za Mirerani Salome Mnyawi na Endiamtu Lucas Zacharia kukaa pamoja juu ya mikakati ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Mirerani.
“Mkurugenzi ameshasema kituo kipya cha afya cha kata ya Mirerani kinapaswa kujengwa mara moja hivyo kaeni kwa pamoja mfanikishe hilo ili kazi ianze,” amesema Kanunga.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi amesema kata hiyo haina zahanati wala kituo cha afya cha serikali ila kuna zahanati mbili za binafsi ya Minja na Moipo zinazohudumia wananchi.
“Wananchi wa kata ya Mirerani hawana kituo cha afya, tunaiomba halmashauri itekeleze sera ya serikali ya kuwa na kituo cha afya kwenye kila kata,” amesema Salome.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia amesema eneo lipo la kujenga kituo cha afya kwenye kata ya Mirerani, hivyo maandalizi yaanze ili kituo hicho kianze kujengwa ili kikamilike.
“Ujenzi wa kituo hicho cha afya kwenye kata ya Mirerani kitapunguza wingi wa wagonjwa kwenye kituo cha afya kilichopo kata ya Endiamtu,” amesema.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian amesema serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer aliyejenga shule.
“Bilionea Laizer amejenga shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza na kuikabidhi serikali hivyo halmashauri imuunge mkono kwa kujengwa bweni,” amesema Taiko.