******************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
WAKULIMA 25 wa Mkoa wa Manyara, wamenufaika na mkopo wa matrekta 25 ya thamani ya shilingi bilioni 1.3 kwa lengo la kuboresha kilimo chao na kuongeza tija Kwa kila mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amekabidhi matrekta hayo 25 yaliyotolewa na kampuni ya PASS Leasing Ltd, kwa wakulima hao mji mdogo wa Katesh.
Makongoro amesema matrekta hayo yataboresha uchumi wa wakulima hao na mkoa mzima wa Manyara kwani hivi sasa watalima kwa tija.
“Nimpongeze mkulima mmoja Marco Mamoya ambaye amesema wakulima hawasubiri maelekezo mara baada ya kupata matrekta ni kuelekea shambani,” amesema Makongoro.
Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja amesema eneo hilo ni nchi ya maziwa na asali hivyo anatarajia wakulima hao watanufaika kupitia kilimo cha mazao mbalimbali.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Hanang’ Mathew Darema amesema wakulima wa eneo hilo ni walipaji wazuri wa mikopo ya matrekta kwani kuna baadhi yao walikopa awamu ya kwanza wakalipa na sasa wanakopa awamu ya pili.
Mmoja kati ya wakulima waliochukua mkopo wa trekta John Marco amesema mkopo huo wa trekta moja ya shilingi milioni 70 utarejeshwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu baada ya kulipia asilimia 20.
Mkurugenzi wa kampuni ya PASS Leasing Ltd, Killo Lussewa amesema hadi hivi sasa kwenye mkoa huo wameshatoa mikopo ya zana za kilimo za thamani ya shilingi bilioni 1.3.
Lussewa amesema kwenye mkoa wa Manyara, wametoa ajira kwa watu 513.
Amesema wameongeza matumizi ya zana bora za kilimo kwa wakulima wa mkoa huo kwani trekta moja ina uwezo wa kulima ekari 12 kwa siku.