Spika Mstaafu wa Bunge Anna Makinda,akitoa mada ya uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya sensa kwa Asasi za Kiraia Katika Mkutano wa wiki ya AZAKI unaoendelea Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society(FCS), Francis Kiwanga,akizungumza wakati wa mada ya uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya sensa kwa Asasi za Kiraia Katika Mkutano wa wiki ya AZAKI unaoendelea Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng’wanakilala, akiwa kwenye picha ya pamoja na wazungumzaji na Baadhi ya watendaji wa LSF mara baada ya kumalizika kwa Mkutano huo.
…………………………………………………………….
Na.Alex Sonna, Dodoma.
Kamisaa wa Sensa ya mwaka 2022, ambaye pia ni Spika wa Bunge Mstaafu Bi. Anna Makinda amezitaka Asasi za kiraia nchini(AZAKI) kushirikiana na Serikali kuhamasisha na kutoa Elimu sahihi ya Sensa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi lililopangwa kufanyika ifikapo Agosti 2022 nchi nzima.
Aidha amezitaka AZAKI hizo kushirikiana na Serikali kuondoa taarifa za kupotosha kwa umma kuhusu zoezi la sense kwani kuna baadhi ya watu hawana elimu sahihi ya sense.
Bi. Makinda ameyabainisha hayo leo Octoba 27, 2021 wakati akitoa mada ya uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya sensa kwa Asasi za Kiraia Katika Mkutano wa wiki ya AZAKI unaoendelea katika Jiji la Dodoma.
Ambapo amesema kuwa umuhimu wa sensa unagusa kila nyanja hivyo ni wajibu kwa kila mtanzania kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.
“Sensa ni muhimu na inafanyika kila baada ya miaka kumi,ninyi watu wa AZAKI ni wadau namba moja kwa kuwa mpo kila sehemu hapa nchini, tunatakiwa kutoka kwenye uchumi wa kati tuende mbali zaidi tufanane na nchi nyingine,”amesema Bi. Makinda.
Amesema Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2012 hivyo Sensa ya mwaka huu itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Ameongeza kuwa “Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum,kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi” Amesema.
Amesema Sensa ya mwaka 2022 inautofauti kidogo kwa kuwa kuna madodoso yameongezwa pia itahusisha umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.
Amebainisha kuwa takwimu hizo ni za msingi ndiyo zitakazowezesha kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
“Taarifa za sensa zitawezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira,msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia,takwimu hizi zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS) Francis Kiwanga, amesema kuwa wao kama Asasi za Kiraia wamejipanga vyema kuhakikisha wanashirikiana na Serikari katika kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kutokana na mashirika ya Asasi za Kiraia kuwa karibu na wananchi kuanzia ngazi ya mashina, kata, vijiji na wilaya kupitia miradi mbalimbali wanayoisimamia kwenye maeneo hayo.
“Tumefurahi kupata hiyo hamasa ambayo imetolewa vizuri sana na wataalamu na hasa sasa hivi Taifa letu linachangamoto ya kutoaminiana hasa kwenye mambo ya msingi kwahiyo sisi kama Asasi za Kiraia ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunatoa elimu sahihi ya wananchi kueliwa umuhimu wa zoezi hili la sensa ya Kitaifa lakini pia elimu ya wananchi kushiriki zoezi hili muhimu la Sensa ya Kitaifa”
Aidha ameeleza namna ambavyo wao kama Asasi za kiraia watakavyoshiriki kuifikia jamii na kuihamasha kushiriki kikamilifu zoezi hilo na kusema kuwa Asasi nyingi zipo vijijini hivyo ni rahisi wao kuifikia jamii husika kwakuwa wao ni miongoni mwa wananchi wanaoshiriki nao kwenye miradi mbalimbali ya huduma za kijamii na maendeleo.
“Tunasema mbuzi kafia kwa muuza supu’ majukumu kama haya sisi ndio tuna uwezo mkubwa wa kuyasukuma na ndio nguvu yetu sisi kama Asasi ule ukaribu na wananchi na tunaamini kwenye hili taarifa sahihi zitafika kwa wananchi” amesema Kiwanga.
Awali Mtakwimu Mwandamizi, kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) David Mwaipopo amesema AZAKI inafasi inanafasi ya wananchi kuwa sensa ya mwaka 2022 kama zilivyo sensa zilizopita itatumia aina mbili kuu za madodoso ambazo ni dodoso refu litakalotumika kuhoji asilimia 30 ya maeneo yote ya kuhesabia watu na Dodoso fupi litakalotumika kuhoji kwenye asilimia 70 ya maeneo yote ya kuhesabia watu.
Ameyataja madodoso mengine kuwa ni la Taasisi ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wasafiri, waliolala mahotelini/nyumba za wageni, na waliolazwa hospitalini na dodoso la Wasio na Makazi maalum ambalo ni mahsusi kwa watu wote wanaolala maeneo yasiyo rasmi, kwenye baraza za majengo mbalimbali, kwenye madaraja na maeneo mengine.
“Utekelezaji wa sensa ya watu na makazi hufanyika katika awamu kuu tatu kuu ambazo ni kipindi kabla ya kuhesabu watu, wakati wa kuhesabu watu na kipindi baada ya kuhesabu watu,”amesema.