Home Mchanganyiko CWT IRINGA VIJIJINI WAMEMPONGEZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KWA KUWAPANDISHA MADARAJA

CWT IRINGA VIJIJINI WAMEMPONGEZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KWA KUWAPANDISHA MADARAJA

0

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na walimu ambao wamehudhuria mafunzo hayo

Mwenyekiti wa CWT Iringa Vijijini mwalimu Saimon Mnyawami Akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu wa wilaya ya Iringa vijijini akiwa sambamba na viongozi wengine

Baadhi ya walimu waliohudhuria nafunzo hayo wakiwa na furaha tere

Na Fredy Mgunda,Iringa.

CHAMA cha walimu wilaya ya Iringa vijijini (CWT)
wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan kwa kuwapandisha madaraja na kuongeza ajira za walimu kwa kipindi kifupi
ambacho yupo madarakani.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu wa wilaya ya Iringa
vijijini,Mwenyekiti wa CWT Iringa Vijijini mwalimu Saimon Mnyawami alisema kuwa
walimu wanafura kubwa kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajali
kwa kuwapandisha madaraja ambayo yanasaidia kuongezeka kwa mshahara.

Alisema kuwa walimu wote 1032 waliopandishwa madaraja
wamesharekebishwa mishahara tangu mwezi wa sita na mwezi wa saba na wapo tayari
kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan kwa kila jambo hata akisema atagombea urais  2025 basi watamuunga mkono.

Mnyawami alisema kuwa walimu wote 2244 wa wilaya ya Iringa
vijijini watashiriki vilivyo kutoa elimu ya sensa ambayo itafanyika mwakani kwa
kuwa zoezi la sensa  litasaidia katika
mipango ya serikali kwasababu watakuwa wanajua idadi ya wananchi wa maeneo
husika.

Alisema kuwa zoezi la sensa ni muhimu sana kwa taifa kujua
idadi ya wakazi kwa ajili ya kupanga mipango ya kuleta maendeleo kwa wananchi
hivyo jukumu la walimu kumuunga mgono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia 100.

Aidha Mnyawami alikemea vitendo vya baadhi ya walimu kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi jambo ambalo linachafua taswira ya kada hiyo
ya walimu hivyo walimu wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi yao.

Alisema kuwa walimu wanapaswa kuendelea kutoa elimu ya
madhara ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii ambazo wanaishi nazo huku ili kuwa
na kizazi ambacho kitakuwa na maadili bora nakutomeza kabisa maswala yote ya
ukatili wa kijinsia.

Mnyawami alisema walimu wanatakiwa kuendelea kuwa na maadili
bora ili kuwasaidia wananchi wengine kuiga mfano wao kwa namna ya kufanya kazi
kwa kujituma na kulijenga taifa kiuchumi na kielimu.

Alisema kuwa rushwa ni adui wa maendeleo ya wananchi wote
hivyo walimu wanatakiwa kuwa matari wa mbele kuhakikisha wanapinga vitendo
vyote vyenye viashiria vya rushwa.

Mnyawami alimalizia kwa kumuomba mkuu wa wilaya ya Iringa
Mohamed Hassan Moyo kufikisha ujumbe wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa walimu wa wilaya ya Iringa
vijijini wanaiunga mkono serikali ya awamu ya sita kutokana na kazi ambayo
wanaifanya.

 Akifungua mafunzo kwa waalimu wawakilishi mahali pa kazi
yanayoendeshwa na chama cha Waalimu Wilaya ya Iringa Vijijini (CWT),Mkuu wa
wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka
walimu kuwa mabalozi wa kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi yao
ikiwemo kujihusisha kingono na wanafunzi kwani tabia hiyo inadharirisha taaluma
yao.

 Moyo alisema kuwa waalimu wenye maadili ni lazima wajikite
kwenye uzalendo na uadilifu ili kuwa mfano bora kwa jamii

Alisisitiza kuwa viongozi wa CWT wanatakiwa kuweka mikakati
ya kuwabaini waalimu wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi ili kukomesha tabia
hiyo ya unyanyasaji na ukatili unaokatisha ndoto za wanafunzi hasa wa kike

 Moyo alisema kuwa ni aibu kusikia mwalim ana mahusiano ya ki
ngono na mwanafunzi jambo hilo limekuwa likiitia doa kada ya ualimu kwa vitendo
amvyo  vinafanywa na baadhi ya walimu kwa
wanafunzi.

“Kama wewe ni kidume wa ukweli nenda kwenye bar na vilabuni
katafute wanawake kule mbona wapo wengi kwanini ukimbilie kwa wanafunzi na
kuwaharibia ndoto zao”alisema Moyo

 alisisitiza kuwa waalimu wote wanatakiwa kuwa mfano bora wa
kuigwa na jamii kwa  kukemea vitendo vya
ukatili na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

 Aidha Moyo alizungumzia changamoto za maslahi kwa waalimu na
kuwahakikishia kuwa Serikali inazitambua na inazifanyia kazi kwa awamu

 Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Chama cha
waalimu CWT yamelenga kuwajengea uwezo waalimu wa wakilishi kutoka shule zote
za wilaya ya Iringa juu ya Masuala ya Sheria za kazi, wajibu wa waalimu na
namna bora ya kushughulikia migogoro mahala pa kazi.