Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akihutubia kwenye Mkutano wa Uzinduzi wa ‘Middle East Green Initiatives’ uliofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia
Washiriki wakifuatilia Mkutano wa Uzinduzi wa ‘Middle East Green Initiatives’ uliofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo (wa pili kushoto) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Saudia, Mhe. Ali Jabir Mwadini (kushoto) na viongozi wengine walioshiriki Mkutano wa Uzinduzi wa ‘Middle East Green Initiatives’ uliofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia jana.
…………………………………………………………….
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Tanzania imejidhatiti katika kujenga uchumi wa kijani na kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Jafo amesema hayo jana katika Mkutano wa Uzinduzi wa ‘Middle East Green Initiatives’ uliofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia na kuhudhuriwa na viongozi wa mataifa mbalimbali na mashirika ya kimataifa.
Waziri Jafo alisisitiza kuwa Tanzania imejipanga kutekeleza uchumi wa kijani kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo matumizi ya nishati jadidifu kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kama vile Mradi wa umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake Mwana Mfalme Mohammed Bin Salman alisema Saudi Arabia na Mataifa ya Mashariki ya Kati yameanzisha Mpango wa ‘Middle East Green Initiative’ kwa lengo la kushirikiana na mataifa mbalimbali katika kukuza uchumi wa kijani na kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kujenga uchumi endelevu.
Mkutano huo ulioandaliwa na Serikali ya Saudi Arabi, uliongozwa na Mwana Mfalme na Makamu Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman.