****************************
NJOMBE
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameungana na wakazi wa mji na mkoa wa Njombe kuombeleza kifo cha mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Romanus Mayemba(CCM) ambaye alianza kusumbuliwa na maradhi mwanzoni mwa mwaka jana.
Akiwasilisha salamu za pole na rambirambi jana kutoka Rais Samia ,katibu wa NEC uchumi na fedha CCM taifa Dkt Frank Hawasi Haule katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe nyumbani kwake Msete alisema Rais ameguswa na kifo cha kiongozi huyo mnyenyekevu
“Mwenyekiti wa chama pamoja katibu mkuu wamenituma kuwapa pole na msiba huu ni wetu sote,kiongozi huyu ni wa kuigwa na watu wote na kuendelea kudumisha amani,Mayemba alifanya kwa nafasi yake na sisi tuwe wema ili tujaze umati kama huu”alisema Haule.
Naye mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya alisema serikali ya mkoa imepokea kwa masikitiko makubwa na kwamba kiongozi huyo alikua namba moja kuhimiza maendeleo.
Akisoma historia ya marehemu na Tadey Luoga ambaye mwakilishi wa halmashauri ya mji wa Njombe pamoja na Efrem Mayemba ambaye ni msemaji wa familia walisema alipokuwa ICU alitoa kauli iliyoonyesha amejiandaa na maisha mapya baada ya kifo.
“Halmashauri ya mji ya Njombe imepoteza kiongozi mahili sio tu kiongozi alikua kama baba kwetu alitulea ,kifo chake ni pigo kubwa sana kwetu”alisema Tadey Luoga.
Katika mazishi hayo vyama vya upinzani navyo wameshiriki ambapo mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Rose Mayemba alisema maisha ya duniani ni mafupi hivyo viongozi wanapaswa kuwa wamoja.
Naye shehe wa mkoa wa Njombe Rajabu Msigwa aliwataka wakazi wa mkoa wa Njombe kuungana kwa pamoja kumuombea marehemu ili aweze kupumzika kwa amani.
Romanus Mayemba alifariki oktoba 24 katika hospitali ya Benjamini Mkapa Iliyopo jijini Dodoma na kisha mwili wake kupumzishwa octoba 26 nyumbani kwake Msete